Iran: Mlango wa kuhuisha JCPOA hautabaki wazi daima
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameionya Marekani kuwa, mlango wa mazungumzo ya kuhuisha makubaliano ya nyukia ya JCPOA hautabaki wazi milele, na kwa msingi huo ameiasa Washington kutumia fursa hiyo vizuri na kuyanusuru mapatano hayo.
Hossein Amir-Abdollahian amesema hayo katika mahojiano na kanali ya CNN na kuongeza kuwa, "Tumeiambia Marekani kupitia wapatanishi kuwa, washirika wa JCPOA wapo katika mkondo wa kufikia makubaliano, lakini hilo linaweza kubadilika iwapo Washington itakengeuka."
Amir-Abdollahian amesema, "dirisha la fursa kwa Marekani la kuhuishwa mapatano ya JCPOA lipo wazi hivi sasa, lakini halitabakia wazi milele."
Amebainisha kuwa, uhusiano wa Iran na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) upo katika hali ya kawaida na ya kuridhisha, lakini iwapo Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) itapasisha sheria mpya, basi hatutakuwa na budi isipokuwa kufungamana na sheria hiyo.
Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran amesisitiza kuwa, mlango wa mazungumzo bado uko wazi na bado Tehran inaendelea kubadilishana ujumbe mbalimbali na pande husika za mazungumzo hayo kupitia wapatanishi.
Amebainisha kuwa, iwapo Marekani na nchi za Ulaya zitaendelea kujikokota katika mazungumzo ya kufufua JCPOA, basi Jamhuri ya Kiislamu karibuni hivi itachukua hatua nyingine mpya za kupunguza uwajibikaji wake katika mapatano hayo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amebainisha kuwa, Marekani kwa upande mmoja inaitumia Iran ujumbe chanya kupitia njia za diplomasia, lakini kwa upande mwingine inatoa matamshi ya hadaa na ya kukanganya kupitia vyombo vya habari.