Marais Raisi na Putin wazungumzia uhusiano wa kiuchumi wa Iran na Russia
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i94814-marais_raisi_na_putin_wazungumzia_uhusiano_wa_kiuchumi_wa_iran_na_russia
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Ebrahim Raisi na mwenzake wa Russia, Vladimir Putin wamesisitizia umuhimu wa kuchukua hatua za kuimarisha zaidi uhusiano wa kiuchumi kati ya nchi mbili hizi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 06, 2023 23:29 UTC
  • Marais Raisi na Putin wazungumzia uhusiano wa kiuchumi wa Iran na Russia

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Ebrahim Raisi na mwenzake wa Russia, Vladimir Putin wamesisitizia umuhimu wa kuchukua hatua za kuimarisha zaidi uhusiano wa kiuchumi kati ya nchi mbili hizi.

Katika mazungumzo yao kupitia njia ya simu jana Jumatatu, Marais hao wamesema kuwa, ushirikiano wa kiuchumi kati ya Iran na Russia unaendelea kuimarika na kustawi.

Kwa mujibu wa shirika rasmi la habari la Iran IRNA, hii ni mara ya tatu kwa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Ebrahim Raisi na mwenzake wa Russia, Vladimir Putin kuwasiliana kwa njia ya simu katika kipindi cha miezi michache iliyopita.

Shirika la habari la TASS la Russia limeashiria mazungumzo ya jana ya Rais Raisi na Rais Putin na kuripoti kuwa, Tehran na Moscow mwaka 2000 zilifikia makubaliano ya kutengenezwa korido ya kimataifa ya kistratajia ya (INSTC), ambayo itaziunganisha Russia na India kupitia ardhi ya Iran.

Ramani inayoonesha njia ya kimkakati ya Kaskazini-Kusini 

Kwa mujibu wa shirika la habari la TASS, kuundwa kwa njia hiyo ya kimkakati ya Kaskazini-Kusini kutapunguza kwa asilimia 50 masafa ya kuziunganisha nchi mbili hizo.

Sayyid Raisi na Rais Putin wameeleza kuwa, kutumiwa fursa na uwezo zilionao Tehran na Moscow, mbali na kudhamini maslahi ya nchi mbili, kunaweza pia kudhamini maslahi na manufaa ya kikanda.