Tehran, mwenyeji wa kongamano la kubainisha ubaguzi na jinai za Israel
Kongamano la kupambana na ubaguzi na jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina lilifanyika jana Jumanne hapa Tehran, mji mkuu wa Iran na kuhudhuria na wajumbe wa makundi ya muqawama ya Palestina, maafisa wa Jamhuri ya Kiislamu na wa nchi kadhaa za Kiarabu.
Akihutubia katika kongamano hilo, Nasser Abu Sharif, mwakilishi wa Harakati ya Jihadul Islami ya Palestina amesema utawala haramu wa Israel umeshadidisha ubaguzi wa rangi 'apartheid' dhidi ya Wapalestina, kwa kuendeleza ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu.
Sharif amesema utawala huo pandikizi ambao hauheshimu sheria zozote za kimataifa, unazidi kupata utajiri kwa kupora mali za wananchi madhulumu wa Palestina.
Wakati huohuo, Katibu Mkuu wa kamati iliyoandaa mkutano huo hapa mjini Tehran, Alireza Karimian amesema katika miongo ya hivi karibuni, uso unaochukiza wa utawala huo unaoua watoto wadogo umezidi kudhihiri kwa uhalisia wake machoni pa walimwengu.
Karimian ameeleza bayana kuwa, kuna haja ya kubainisha na kuanika sera za kibaguzi na jinai za utawala huo haramu dhidi ya Wapalestina wasio na ulinzi, ili kuwatanabahisha walimwengu wote.
Wanajeshi wa utawala ghasibu unaoikalia Quds Tukufu na Masjidul Aqsa kwa mabavu wameshadidisha hujuma zao katika wiki za hivi karibuni, huku wakiwalenga kwa risasi za moja kwa moja raia wa Palestina wasio na ulinzi hasa katika miji ya Jenin na Nablus katika eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
Takwimu za Wizara ya Afya ya Palestina zinaonesha kuwa, Wapalestina karibu 90 wakiwemo watoto wadogo 15 wameuawa shahidi na jeshi la utawala haramu wa Israel tangu kuanza mwaka huu wa 2023, hasa katika maeneo ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.