Mkuu wa IRGC: Israel itaporomoka na Palestina itapata uhai mpya
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i96280-mkuu_wa_irgc_israel_itaporomoka_na_palestina_itapata_uhai_mpya
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) anasema kuwa utawala wa Israel uko karibu kuporomoka huku ukikabiliwa na migogoro kadhaa wakati ambao harakati za ukombozi wa Palestina zinapata uhai mapya.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 14, 2023 23:07 UTC
  • Meja Jenerali Hossein Salami
    Meja Jenerali Hossein Salami

Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) anasema kuwa utawala wa Israel uko karibu kuporomoka huku ukikabiliwa na migogoro kadhaa wakati ambao harakati za ukombozi wa Palestina zinapata uhai mapya.

Meja Jenerali Hossein Salami aliyasema hayo jana Ijumaa alipokuwa akihutubia maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds huko Isfahan, katikati mwa Iran.

Ameongeza kuwa ishara ya kwanza ya kudidimia utawala wa Kizayuni wa Israel ni kwamba utawala huo hauna mfumo imara wa kisiasa.

Jenerali Salami amesema hatua ya baadhi ya tawala za Kiarabu kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel ni "chanzo cha aibu", na kuongeza kuwa tawala ambazo zimefanya hivyo "zitajutia" uamuzi huo kwani zinaelewa kuwa "haziwezi kutegemea msaada wa kitu ambacho kimeliwa na mchwa kutokea ndani ... kwani kitasambaratika hivi karibuni."

Kamanda Mkuu wa IRGC alikuwa akiashiria mapatano ya 'Abraham' yaliyosimamiwa na Marekani, ambayo kwa mujibu wake utawala wa Israel ulianzisha uhusiano wa kidiplomasia na Umoja wa Falme za Kiarabu, Bahrain, Sudan na Morocco mwaka 2020.

Jenerali Salami ameeleza kuwa hivi sasa utawala wa Kizayuni wa Israel unakabiliwa na migogoro kadhaa mikubwa, ikiwa ni pamoja na kutengwa katika sera za kigeni, ukosefu wa utulivu wa ndani, maandamano, na serikali isiyo na ufanisi.

Kamanda Mkuu wa IRGC amesema leo uhai mpya umepulizwa katika harakati za ukombozi wa  Palestina na kuongeza kuwa operesheni za wanamapambano Wapalestina zinafanyika katika Ukingo wa Magharibi na Tel Aviv, na utawala wa Kizayuni umeshindwa kuwazuia Wapalestina kuingiza silaha na kutekeleza mashambulizi katika maeneo hayo.

Maandamano ya SIku ya Kimataifa ya Quds maeneo mbali mbali ya Iran

Matamshi hayo yametolewa huku mamilioni ya Waislamu kote duniani wakiingia barabarani siku ya Ijumaa kupaza sauti zao za kuunga mkono kadhia ya Palestina.

Siku ya Kimataifa ya Quds ni miongoni mwa urithi wa hayati mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Imam Ruhullah Khomeini (MA), ambaye anaenziwa kama kiongozi wa kiroho na Waislamu duniani kote. Ikumbukwe kuwa mwaka 1979, muda mfupi baada ya kuongoza Mapinduzi ya Kiislamu ambayo yalimuondoa madarakani Shah wa Iran anayekuwa akiungwa mkono na Marekani, Ayatullah Khomeini aliitangaza Ijumaa ya mwisho ya mfungo wa mwezi wa Ramadhani kuwa Siku ya Quds.

 Maandamano ya Siku ya Quds ya mwaka huu yamepata umuhimu zaidi huku utawala wa Kizayuni ukiuvunjia heshima Msikiti wa al-Aqsa kwa kuwashambulia Waislamu katika mwezi mtukufu wa Ramadhani katika mipango yake ya kuyahudisha eneo hilo takatifu la Kiislamu.