Jibu la Iran kwa azimio la kiadui la bunge la Uswidi
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran amesema kuwa hatua ya bunge la Uswidi ya kupitisha azimio dhidi ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu IRGC, imeathiriwa na makundi ya kigaidi yaliyokataliwa na taifa la Iran na kwamba ni kinyume na viwango na sheria za kimataifa.
Siku ya Jumatano, bunge la Uswidi lilipitishia azimio ambalo linaitaka serikali ya nchi hiyo kuweka jina la IRGC katika orodha ya makundi yanayotuhumiwa na Umoja wa Ulaya kuwa ya kigaidi.
Nasser Kanani, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran alisema Alkhamisi kwamba Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ni taasisi huru inayotokana na matakwa ya watu wa Iran na ina utambulisho rasmi na wa kisheria unaotokana na Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na ambayo, sambamba na vyombo vingine vya jeshi, ina jukumu la kulinda usalama wa taifa na mipaka ya nchi.
Hatua hiyo ya bunge la Uswidi dhidi ya Iran imechukuliwa huku Bunge la Ulaya likiathiriwa na wapinzani wa Jamhuri ya Kiislamu na pia kufuata siasa za chuki zinazochochewa na Marekani dhidi ya Iran. Tarehe 19 Januari mwaka huu bunge hilo la Ulaya lilipitisha mswada ambao ulitaka kuwekwa jina la Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran katika orodha ya makundi yanayodaiwa kuwa ya "kigaidi" ya Umoja wa Ulaya. Licha ya kuwa umoja huo ulijiepusha kuliweka jina la keshi la IRGC katika orodha ya makundi ya kigaidi baada ya viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kutahadharisha juu ya matokeo mabaya ya hatua kama hiyo, lakini uliwawekea vikwazo vipya baadhi ya maafisa wa jeshi hilo.
Miezi kadhaa iliyopita, nchi za Ulaya zikiwemo Uingereza, Ufaransa na Ujerumani pamoja na Umoja wa Ulaya ziliwawekea vikwazo mara kadhaa makamanda wa kijeshi wa Iran kwa lengo la kuibua machafuko na ghasia nchini, lakini licha ya hatua na njama zote hizo, jeshi, wakiwemo Walinzi wa Mapinduzi, lilishirikiana kwa karibu na wananchi na kutumia busara kubwa katika kuerejesha amani na usalama katika miji tofauti ya Iran.
Ukweli ni kwamba Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu limekuwa na nafasi kubwa katika kulinda usalama nchini na pia katika eneo la Magharibi mwa Asia kutokana na mapambano yake makali dhidi ya makundi ya kigaidi. Mapambano dhidi ya makundi ya kigaidi ya ndani na nje ya nchi, kuanzia munafikina hadi Daesh, ni miongoni mwa juhudi kubwa zilizofanywa na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, ambalo pia limetoa mashahidi wengi kama vile Luteni Jenerali Haj Qassem Soleimani katika njia hiyo. Kwa hivyo, lau kama hazingekuwa ni juhudi za jeshi la IRGC, leo hii eneo lingekuwa linashuhudia machafuko makubwa ya harakati za magaidi, ambazo pia zingeziathiri nchi za Ulaya.
Nukta nyingine muhimu kuhusu hatua ya bunge la Uswidi dhidi ya Iran ni kwamba, hatua hiyo ni mfano wa uingiliaji masuala ya ndani ya nchi na pia ni kinyume cha sheria za kimataifa. IRGC ni sehemu rasmi ya jeshi la Jamhuri ya Kiislamu na vikwazo vyovyote dhidi yake vinachukuliwa kuwa kinyume cha sheria za kimataifa kwa mujibu wa kipengee cha 7, ibara ya 2 ya Hati ya Umoja wa Mataifa.
Ni dhahiri kwamba utendaji kazi wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi katika miongo minne iliyopita, hususan katika kipindi cha vita vya kujitetea kutakatifu, kuzima njama na moto wa fitina za makundi ya kigaidi ya ndani na nje ya nchi, na vile vile kuchangia maendeleo mbalimbali ya nchi ikiwa ni pamoja na utengenezaji wa silaha za kisasa kabisa, yote hayo yanaashiria ukweli kwamba hatua za nchi za Magharibi dhidi ya IRGC hazijaweza kamwe kuzuia juhudi za jeshi hilo katika kulinda usalama na kufikia maendelea yanayoongezeka kila siku ya jeshi hilo shupavu.
Kwa msingi huo, Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran ameishauri serikali ya Uswidi kutumia busara ili kuepuka kutumbukia katika mtego mkubwa unaokusudiwa kuharibu uhusiano wa nchi mbili. Ameitaka kufikiria vizuri madhara ya hatua kama hiyo inayohatarisha maslahi ya taifa la Uswidi na uhusiano wa muda mrefu wa nchi mbili, na kutoutoa muhanga uhusiano huo kwa maslahi ya magaidi, utawala wa kibaguzi wa Israel na maadui wengine wa taifa la Iran.