Zarif: Uhusiano wa Iran na Ufaransa ni kwa maslahi ya dunia
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amesisitiza umuhimu wa kuimarishwa uhusiano kati ya Jamhuri ya Kiislamu na Ufaransa na kusema kuwa ushirikiano huo utachangia kuleta amani na uthabiti duniani.
Katika kikao cha pamoja na waandishi wa habari mjini Paris pamoja na mwenzake wa Ufaransa Jean-Marc Ayrault, Muhammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema Tehran iko tayari kuimarisha uhusiano wa pande mbili na Ufaransa, haswa katika kipindi hiki cha utekelezwaji wa makubaliano ya nyuklia kati ya Iran na nchi za kundi la 5+1, yajulikanayo kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA).
Zarif amepongeza mazungumzo kati yake na Rais Francois Hollande katika Ikulu ya Élysée na kusema kuwa mbali na maswala ya kuimarisha uhusiano wa pande mbili, wawili hao wamejadiliana maswala ya kieneo na kimataifa na kubadiishana mawazo katika mambo tofauti kama vile usalama na amani katika eneo la Mashariki ya Kati na tatizo la ugaidi. Kadhalika Tehran na Paris zimejadiliana kuhusu mkataba wa dola bilioni 27 za Marekani ambapo Iran iliafiki kununua ndege 118 kutoka Shirika la Airbus la Ufaransa.
Wakati huo huo, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amesisitizia utayarifu wa taifa hili katika kutekeleza makubaliano ya nyuklia ya Vienna yaliyoanza kutekelezwa Januari mwaka huu.