Abdollahian akosoa hatua ya Sweden ya kuunga mkono kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i99356-abdollahian_akosoa_hatua_ya_sweden_ya_kuunga_mkono_kuvunjiwa_heshima_qur'ani_tukufu
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amelaani vikali hatua ya Sweden ya kuunga mkono vitendo vya kuvunjiwa heshima matukufu ya dini ikiwemo Qur'ani Tukufu.
(last modified 2026-02-05T12:50:29+00:00 )
Jun 30, 2023 07:25 UTC
  • Abdollahian akosoa hatua ya Sweden ya kuunga mkono kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amelaani vikali hatua ya Sweden ya kuunga mkono vitendo vya kuvunjiwa heshima matukufu ya dini ikiwemo Qur'ani Tukufu.

Hussein Amir-Abdollahian amesema hayo katika ujumbe wake kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter na kusisitiza kwamba, uvunjiaji heshima matukufu ya dini kikiwemo kitabu kitakatifu cha Waislamu cha Qur'ani katu hakikubaliki kwa namna yoyote ile.

Aidha ameongeza kuwa, kuhalilisha vitendo kama hivi kwa kisingizio cha demokrasia na uhuru hakuna natija nyingine ghairi ya kushajiisha vitendo vya kigaidi na misimamo ya kufurutu mpaka.

Hayo yanafuatia hatua ya polisi ya Sweden kutoa kibali kwa raia mmoja wa nchi hiyo kuchoma moto nakala ya Qur'ani Tukufu wakati wa sikukuu ya Idul Adh'ha na serikali ya nchi hiyo imetetea kitendo chake hicho cha kijinai.

Ulimwengu wa Kiislamu umelaani vikali kitendo cha kuvunjiwa heshima Qurani Tukufu (kitabu kitakatifu cha Waislamu) huko nchini Sweden.

Mataifa mengi ya Waislamu kama Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Iraq, Saudi Arabia, Kuwait, Pakistan, Jordan na Uturuki yametoa taarifa za kulaani kitendo hicho cha kishenzi cha kuvunjiwa heshima Qurani Tukufu nchini Sweden.

Wakati huohuo, Morocco imemuita nyumbani Balozi wake kutoka Sweden, kulalamikia jinai hiyo ya kuvunjiwa heshima Qurani Tukufu nchini Sweden.

Aidha Kituo cha Kiislamu cha Al-Azhar cha Misri kimelaani kitendo hicho dhidi ya Qurani Tukufu, na kusema kitendo hicho kimefanywa na watu wenye mfungamano na mrengo wa kulia wa Sweden na kwamba serikali ya Uswidi ni mshirika katika uhalifu huo.