Helikopta za Iran ndizo zenye uwezo mkubwa zaidi Asia Magharibi
Kamanda wa Kikosi cha Anga cha Jeshi la Nchi Kavu la Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu inamiliki helikopta nyingi zaidi, za kisasa na zenye uwezo mkubwa zaidi katika eneo la Asia Magharibi.
Brigedia Jenerali wa Pili, Yousef Qorbani amesema hayo katika mkutano wa waandishi wa habari mjini Tehran na kuongeza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu imepata mafanikio hayo ya kumiliki helikopta zenye uwezo mkubwa zaidi katika eneo licha ya vikwazo vya Wamagharibi.
Amewapongeza wataalamu na wahandisi wa Iran kwa kuzalisha vipuri vya aina yake na vya kisasa zaidi vya ndege hizo za kijeshi, licha ya mashinikizo ya nchi za Magharibi.
Brigedia Jenerali Qorbani ameeleza kuwa, "Helikopta za Jeshi la Iran zimesimikwa makombora ya masafa marefu yenye usahihi mkubwa katika kulenga shabaha. Yakivurumishwa, yanapiga shabaha ndani ya sekunde tatu."
Kamanda wa Kikosi cha Anga cha Jeshi la Nchi Kavu la Iran amebainisha kuwa, taifa hili la Kiislamu limepiga hatua kubwa pia katika uga wa anga za mbali ambao unaendana na wakati.
Kwa mujibu wa Wzaiara ya Ulinzi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, mafanikio iliyoyapata nchi hii katika miongo minne iliyopita yamelifanya taifa hili hii leo liwe na uwezo wa kuzalisha zaidi ya asilimia 90 ya vipuri vya ndege na helikopta.
Wataalamu na wahandisi wa kijeshi wa Iran katika miaka ya hivi karibuni wamepata maendeleo makubwa katika kutengeneza aina mbalimbali za zana za kujihami ndani ya nchi na hivyo kuwezesha majeshi ya Iran kujitosheleza katika silaha.