Jan 02, 2024 02:49 UTC
  • Vituo vya matibabu ya akili vyataka kutangazwa hali ya hatari Israel

Gazeti moja la utawala wa Kizayuni limefichua kuwa, tangu ilipoanza operesheni ya #Kimbunga_cha_al-Aqsa hadi hivi sasa, zaidi ya wakazi laki tatu wa utawala wa Kizayuni wameingia kwenye orodha ya watu wenye matatizo ya akili na saikolojia huko Israel.

Shirika la habari la FARS limelinukuu gazeti la Kizayuni la Yedioth Ahronoth likifichua majanga hayo ya Wazayuni kutokana na vita vya Ghahza na kusema kuwa, madhara ya kiakili katika jamii ya Israel na wanajeshi Wazayuni tangu ilipoanza operesheni ya #Kimbunga_cha_al-Aqsa tarehe 7 Oktoba mwaka ulioisha wa 2023 ni makubwa kiasi kwamba mahospitali na vituo vya matibabu vimeitaka serikali ya Netanyahu itangaze hali ya hatari huko Israel.

Kwa mujibu wa gazeti hilo, Wazayuni wasiopungua laki tatu wamesajiliwa na vituo vya afya na hospitali za utawala wa Kizayuni kuwa na maradhi ya akili na vituo hivyo vya afya vimetangaza kwamba, kuna udharura wa kutangazwa hali ya hatari kutokana na mgogoro mkubwa wa matatizo ya akili kwa "Waisraeli."

Uugonjwa wa akili umewasakama wanajeshi wa Israel

 

Vituo vya matibabu ya akili vya Israel aidha vimesema kwenye barua yao kwamba, mfumo wa matibabu ya akili wa utawala wa Kizayauni umekaribia kusambaratika tena wakati huu ambapo kwa miaka kadhaa sasa vituo vya afya vya Israel vina matatizo ya bajeti na kukosekana wafanyakazi wa tiba na afya.

Kwa upande wake, tovuti nyingine moja ya utawala wa Kizayuni imesema kuwa, tangu tarehe saba Oktoba 2023 wakati ilipoanza operesheni ya #Kimbunga_cha_al-Aqsa hadi hivi sasa,  karibu wanajeshi 2000 wa Israel wamekwenda kwenye vituo vya matibabu kutibiwa magonjwa ya akili. 

Tovuti hiyo ya Kizayuni pia imesema, karibu asilimia 80 ya wanajeshi wa Israel waliokwenda kuomba matibabu ya akili kwenye vituo vya matibabu na mahospitali ya utawala wa Kizayuni wamo kwenye orodha ya majeruhi wa vita vya Ghaza.

Kabla ya hapo pia, gazeti jingine la Kizayuni la Haaretz nalo lilikuwa limefichua kwamba, mamia ya wanajeshi wa Israel wamekumbwa na maradhi ya akili tangu vilipoanza vita vya Ghaza.

Tags