Jan 30, 2024 11:29 UTC
  • Wanajeshi wa Israel waliovalia sare za madaktari na wauguzi wamewaua shahidi Wapalestina 3 Jenin

Ripoti kutoka eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan zinaeleza kuwa wanajeshi 10 wa Israel waliokuwa wamevalia sare za madaktari na wauguzi mapema leo Jumanne waliivamia hospitali ya Ibn Sina katika mji wa Jenin na kuwauwa shahidi vijana watatu wa Kipalestina kwa kutumia bunduki zilizowekwa kifaa cha kupunguza mlio wa sauti za risasi.

Shirika la habari la Wafa la Palestina limezinukuu duru kadhaa katika hopistali ya Ibn Sina huko Jenin na kuripoti kuwa, wanajeshi 10 wa utawala wa Kizayuni wa Israel waliojifanya madaktari, wauguzi na raia wa kawaida mapema leo walivamia hospitali hiyo katika mji wa Jenin, kaskazini mwa eneo la Ukingo wa Magharibi linalokaliwa kwa mabavu, na kuwauwa shahidi Wapalestina watatu wakiwemo makaka wawili kwa kutumia bunduki zilizowekwa kifaa cha kupunguza mlio wa sauti za risasi. 

Wapalestina hao watatu waliouliwa shahidi katika hujuma hiyo ya utawala wa Kizayuni katika hospitali ya Ibn Sina wametajwa kuwa ni Mohammad, Basil al Ghazzawi na Mohammad Jalamna. Basil al Ghazzawi aliyekuwa na umri wa miaka 25, alikuwa hopistalini hapo akipatiwa matibabu wakati wanajeshi wa Israel waliposhambulia hospitali hiyo na kumuua shahidi.  

Katika video iliyosambaa kwenye mtandao wa kijamii wa X, wanajeshi wa Israel wanaonekana wakifyatua bunduki na kuwatishia wafanyakazi na wagonjwa ndani ya hospitali hiyo ya Ibn Sina. Mmoja wa wanajeshi hao, aliyevalia nguo nyeusi kabisa, anaonekana akimlazimisha Mpalestina kupiga magoti huku mikono yake ikiwa imeinuliwa juu.

Mai Alkaila Waziri wa Afya wa Palestina ameuhimiza Umoja jwa Mataifa na makundi ya kimataifa ya haki za binadamu kuhitimisha jinai za kila siku za utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya wakazi wa Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi ikiwa na pamoja na kuzilinda taasisi za afya mbele ya mashambulizi. Makundi ya Wapalestina katika mji wa Jenin yameitisha mgomo wa umma kulalamikia mauaji  hayo ya Wapalestina hospitalini.   

Hujuma na mashambulizi ya wanajeshi wa utawala wa Kizayuni Ukingo wa Magharibi 

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Palestina, wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel wamewauwa shahidi Wapalestina 380 katika Ukingo wa Magharibi tangu Oktoba 7 mwaka jana, huku wengine zaidi ya 4,000 wakijeruhiwa.

Tags