Feb 23, 2024 08:27 UTC
  • Idhini mpya ya Uingereza kwa Israel ya kuendeleza mauaji ya umati dhidi ya wananchi wa Palestina

Uingereza ambayo ni moja ya waungaji mkono wakuu wa jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina sambamba na Ujerumani na Marekani, hivi sasa imetoa idhini mpya kwa Israel ya kuendeleza mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina hasa wa Ghazza. Madola hayo matatu ya Magharibi ndiyo yaliyoko mstari wa mbele katika kuusheheneza silaha hatari utawala wa Kizayuni ili uzidi kuua raia wa Palestina hasa wanawake na watoto wadogo.

Hii ni kusema kuwa, Mahakama Kuu ya London, imekataa ombi la kuiamrisha serikali ya Uingereza iache kuipa silaha Israel. Hukumu hiyo imetolewa baada ya muungano wa makundi ya haki za binadamu kufungua kesi mwezi Januari 2024 na kuitaka mahakama hiyo iizuie serikali yenye misimamo mikali ya Uinngereza isiendelee kulipa vipuri vya silaha jeshi la utawala wa Kizayuni kwani kufanya hivyo kunahatarisha usalama wa dunia nzima na kunakanyaga sheria za kimataifa. Mawakili wa makundi ya haki za binadamu wameamua kukata rufaa kupina hukumu ya Mahakama Kuu ya London ya kukataa kuipiga marufuku serikali ya Uingereza kuipa silaha Israel.

Mwaka 2022, Uingereza iliipa Israel silaha zenye thamani ya dola milioni 53 vikiwemo vipuri vya ndege, zana za kivita, makombora pamoja na silaha nzito na nyepesi.

Lakini baada ya utawala wa Kizayuni kushadidisha jinai zake dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Ghazza, Uingereza imezidisha kiwango cha silaha hizo inazotoa kwa Israel. Makundi ya kupigania haki za binadamu yamefungua mashtaka mara kadhaa kujaribu kuizuia Uingereza na madola mengine ya Magharibi yasiendelee kuisheheneza silaha Israel, lakini hadi hivi sasa London inaendelea kuupa utawala katili wa Kizayuni silaha kali za kuulia Wapalestina. Katikati ya mwezi huu wa Februari, Mahakama ya Kimataifa ya The Hague ilitoa hukumu ya kuipiga marufuku Uholanzi iache kuipa Israel vipuri vya ndege za kivita za F35 kwani ndege hizo zinatumika kufanya mauaji ya halaiki dhidi ya wananchi wa Ghazza. Mahakama hiyo ilisema, ndege hizo zinatumika kuvunja sheria za kimataifa na zinasababisha hatari za wazi kabisa duniani.

Marekani, Uingereza na Ujerumani ziko mstari wa mbele kuunga mkono mauaji ya raia na jinai za Israel huko Ghazza, Palestina

 

Hatua mpya ya Uingereza ni muendelezo siasa kuu ya dola hilo la kiistikbari kuhusu kuuunga mkono utawala wa Kizayuni kwa hali yoyote ile. Uingereza ni muitifaki mkubwa wa Marekani na mara zote madola hayo ya kibeberu ya Magharibi ni waungaji mkono wakuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel. Madola hayo yanaiunga mkono Tel-Aviv kibubusa na kwa hali zote. Madola hayo ndiyo yaliyoipa silaha za nyuklia Israel na ni Uingereza ndiyo iliyofungua njia za kuporwa Wapalestina ardhi zao na kuundwa ndani ya ardhi hizo, dola pandikizi la Kizayuni lililopachikwa jina la Israel na hadi leo zinaendelea kuusheheneza silaha za kila namna utawala huo ili uendelee kuwaua kwa umati wanawake, vizee, watoto wadogo na raia wa kawaida wa Palestina hasa huko Ghazza.

Baada ya operesheni ya Kimbunga cha al Aqsa hapo tarehe 7 Oktoba 2023 na kuanza mashambulizi ya pande zote ya kikatili ya Israel dhidi ya Ghazza, nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani, Uingereza na Ujerumani zimezidi kuonesha uadui wao kwa Wapalestina kwa kuunga mkono kwa nguvu zao zote jinai za utawala wa Kizayuni. Waziri mkuu wa Uingereza, Rishi Sunak, rais wa Marekani, Joe Biden na kansela wa Ujerumani, Olaf Scholz, walitangaza waziwazi mwanzoni kabisa mwa jinai mpya za Israel huko Ghazza kwamba wanaunga mkono jinai hizo hadi pale harakati ya HAMAS itakapofutwa kabisa.

Hivi sasa na baada ya mashambulizi ya Ghazza kuingia mwezi wake wa tano tena, utawala wa Kizayuni umekusudia kuanzisha vita vya nchi kavu dhidi ya eneo la Rafah la kusini mwa ukanda huo. Lakini malalamiko na mashinikizo ya walimwengu dhidi ya jinai hizo ni makubwa sana kiasi kwamba yameilazimisha serikali ya kibeberu ya Uingereza ifanya njama za kujaribu kuhalalisha uvamizi huo. Ingawa kuna madai kuwa, London imetishia kupunguza silaha inazoipa Israel iwapo itaanzisha vita vya nchi kavu huko Rafah, lakini muda wote madola ya Magharibi hayaachi kuunga mkono kibubusa jinai za utawala wa Kizayuni.

Jinai za Israel dhidi ya Wapalestina hazina kifani, na isingeliweza kukfanya jinai hizo zote kama si uungaji mkono wa madola ya kibeberu yanayoongozwa na Marekani, Uingereza na Ujerumani

 

Rafah ni mji wenye ukubwa wa kilomita mraba 55 na uko kwenye mpaka wa Ghazza na Misri. Zaidi ya nusu ya wakazi wa kaskazini mwa ukanda huo wamekimbilia Rafah baada ya Israel kuanzisha mashambulizi ya kikatili tarehe 7 Oktoba 2023. Ni wazi kuwa iwapo Wazayuni wataanzisha mashambulizi ya nchi kavu kwenye mji huo, watasababisha maafa mengine makubwa ya kibinadamu.

Hukumu ya Mahakama Kuu ya Uingereza ya kupinga ombi la kuiamrisha serikali ya Uingereza iache kuupa silaha utawala wa Kizayuni, kwa kweli imeifedhehesha nchi hiyo ya kibeberu na imezidi kuthibitisha uongo wa madai yake kuwa huenda ikapunguza kuipa silaha Israel iwapo itaanzisha mashambulizi ya nchi kavu huko Rafah. Lakini nyoyo za watu wenye hisia za ubinadamu haziko pamoja na viongozi na watawala wa madola ya kibeberu. Katika miezi ya hivi karibuni, mji mkuu wa Uingereza, London umeshuhudia maandamano ya mamia ya maelfu ya watu wanaopinga jinai za Israel huko Palestina na kuhimiza kusimamishwa vita na kukomeshwa mara moja mauaji ya kimbari kwenye Ukanda wa Ghazza.

Tags