Mar 18, 2024 11:13 UTC
  • HAMAS: Muqawama wa kupambana na Israel umevuka mipaka ya Ghaza

Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS imesema utawala wa Kizayuni wa Israel unakabiliwa na "safu pana zaidi" ya Muqawama iliyovuka mpaka wa Ukanda wa Ghaza.

Mwakilishi wa Hamas nchini Lebanon, Osama Hamdan ameiambia televisheni ya Al-Manar ya Lebanon ya kwamba mipaka ya uwanja wa vita haikomei Ghaza na adui anajikuta amekabiliana na safu pana zaidi ya Muqawama.

Utawala wa Kizayuni ulianzisha vita dhidi ya Ghaza Oktoba 7, 2023 kufuatia operesheni ya kulipiza kisasi ya makundi ya Muqawama ya eneo hilo. Tangu lilipoanzisha vita hivyo vya mauaji ya kimbari, jeshi la Kizayuni hadi sasa limeshaua shahidi zaidi ya Wapalestina 31,600 wa Ukanda wa Ghaza, wengi wao wakiwa wanawake, watoto na vijana wadogo.

Katika kukabiliana na jinai hiyo, harakati za Muqawama za Lebanon, Iraq na Yemen zimekuwa zikifanya operesheni za kijeshi dhidi ya utawala wa Tel Aviv na maslahi yake katika eneo.

Osama Hamdan

Katika mahojiano hayo na Al-Manar, Hamdan amebainisha pia kuwa, licha ya kuendesha kampeni ya mauaji makubwa ya kimbari na uharibifu usio na mfano, adui Mzayuni ameshindwa kufikia hata moja kati ya "malengo" yake yote aliyojiwekea.

Kauli ya kiongozi huyo ya mwandamizi wa Hamas inaashiria malengo yaliyotangazwa na Israel ya kuhakikisha inawakomboa mateka wake wote wanaoshikiliwa na Muqawama wa Palestina, kuwalazimisha wakazi wa Ghaza walihame eneo hilo kuelekea nchi jirani ya Misri, na "kuiangamiza" Hamas.

Hamdan amesema: "baada ya siku 163, Muqawama ungali unao uwezo wa kupambana katika uwanja wa vita".

Katika sehemu nyingine ya mahojiano hayo, kiongozi huyo mwandamizi wa Hamas amesema, Muqawama ungali unapambana katika maeneo yote, wakati jeshi la Israel linadai kuwa limeshamaliza vita na kuuangamiza Muqawama, jambo ambalo limezusha migogoro kwa jeshi hilo la utawala wa ghasibu wa Kizayuni.../

Tags