Apr 09, 2024 02:18 UTC
  • Watoto ndio wahanga wakuu wa vita vya Gaza

Katika siku za hivi karibuni vyombo tofauti vya Umoja wa Mataifa vimechapisha ripoti mpya kuhusu kuharibika zaidi hali ya kibinadamu huko Gaza hususan ya watoto, jambo ambalo linaifanya kadhia ya jinai za kivita za jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel kupata uzito zaidi.

James Elder, Msemaji wa Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) amesema: Watoto 600,000 huko Rafah, kusini mwa Ukanda wa Gaza wanakabiliwa na njaa, wanaishi kwa hofu na kukabiliwa na hatari ya kulengwa wakati wowote na majeshi ya Israel. UNICEF imesambaza video ya Elder akizungumzia mateso ya watoto wanaoendelea kuteseka huko Rafah chini ya mashambulizi ya Israel na baada ya watu milioni 1.5 kufukuzwa kwenye makazi yao na askari vamizi wa utawala huo vamizi.

Amesema: "Mtu yeyote ambaye ana hisia za mzazi ambaye ana wasiwasi kuhusu watoto wake au anajali hisia za watoto anapaswa kukomesha mateso haya huko Rafah."

Lynn Hastings, Mratibu wa Masuala ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu (Israel) amesema kuwa, utapiamlo miongoni mwa watoto wa Kipalestina huko Gaza umefikia kiwango cha kutisha na kisicho na mfano wake.

Watoto wa Gaza wanakabiliwa na utapiamlo mkubwa

Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) pia limesema kwamba hali ya usalama wa chakula katika Ukanda wa Gaza ni mbaya sana. Ripoti hizi zinaonyesha wazi kuwa jeshi na utawala wenye misimamo mikali ya kifashisti huko Tel Aviv umeamua kufanya mauaji ya halaiki ya makusudi dhidi ya Wapalestina na ndio maana wengi wa wanaouliwa au kujeruhiwa katika vita vya Gaza ni watoto na vijana wadogo.

Katika kipindi cha miezi sita iliyopita pekee, kati ya wahanga zaidi ya 33,000 wa mauaji hayo ya halaiki, zaidi ya wanga elfu 14 na 350 kati yao ni watoto, ambao ni asilimia 44 ya wahanga wa vita, idadi ambayo inafikia zaidi ya asilimia 70 ikiwa wanawake na akina mama watajumuishwa.

Kwa hakika, vikosi vya uvamizi vinaua watoto wanne katika kila saa huko Gaza, na zaidi ya hayo, zaidi ya watoto elfu 43 na 349 wamepoteza wazazi wao au mmoja wa wazazi, ambapo hawana wa kumkimbilia wanapodondoshewa mabomu vichwani na wavamizi wa Kizayuni. Jambo hilo linawasababishia madhara makubwa ya kisaikolojia na kinafsi. Sasa baada ya kutekelezwa mauaji haya yote ya kutisha dhidi ya watoto wa Kipalestina, je, ni watoto wangapi zaidi wanapaswa kuuliwa kinyama kwa njia hii kabla ya jamii ya kimataifa, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na Baraza la Haki za Binadamu kuchukua hatua ya kuuwajibisha kisheria utawala huo kutokana na jinai hizo za kutisha?

Bila shaka watoto ambao wamenusurika katika mashambulizi na mauaji ya Wazayuni hawana imani ya kuepuka vitisho na hatari nyingine inayowakabili kutoka kwa utawala huo. Ukiukaji wa utawala wa kibaguzi wa Israel kuhusu mfumo mzima wa haki za watoto umeathiri pakubwa haki zao za msingi kama vile haki za kuishi, afya, elimu, maji, chakula na matibabu.

Asilimia 95 ya wakaazi wa Gaza wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula, ambapo hali hiyo ni mbaya zaidi miongoni mwa watoto ambapo watoto walio chini ya umri wa miaka mitano huko Gaza wanakabiliwa na hatari kubwa ya utapiamlo. Watoto, akina mama wajawazito na wanaonyonyesha, na watu wenye ulemavu wako katika hatari zaidi ya utapiamlo, huku utawala haramu wa Israel ukiendelea kuzuia chakula na maji kuingia Gaza, pamoja na kulipua maduka ya kuoka na kuuza mikate na vile vile uzalishaji wa mazao ya kilimo.

Watoto, wahanga wakuu wa jinai za Wazayuni

Vyanzo vya habari na mitandao ya kijamii imechapisha video yenye kutia uchungu inayoonyesha mtoto wa Kipalestina huko Gaza aliyetembea umbali wa kilomita 12 bila viatu kwa ajili ya kutafuta chakula. UNICEF inakadiria kuwa watoto 1,000 huko Gaza wamekatwa viungo tangu mzozo huo uanze mwezi Oktoba. Mashirika ya haki za binadamu, yanaeleza kuwa watoto 10 huko Gaza wanakabiliwa na hatari ya kukatwa miguu kila siku. Yanasema upasuaji na ukataji wa viungo vya watoto hospitalini kwa kawaida hufanyika bila ganzi.

Vilevile, tangu kuanza operesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa, wanajeshi wa Israel wanawazuia gerezani watoto 500 wa Kipalestina, ambapo familia nyingi hazijui hatima ya watoto wao waliokamatwa. Licha ya kuwa ukatili huo wa utawala wa Kizayuni unahesabiwa kuwa jinai za kivita kwa mujibu wa sheria za kimataifa, lakini hatua ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC ya kufumbia macho jinai hizo kumeufanya utawala huo umee pembe na kuendelea kutekeleza ukatili huo bila kujali lolote.

Tags