May 19, 2018 11:17 UTC
  • Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na sisitizo la kuwajibika ulimwengu katika kuunga mkono haki za wananchi  wa Palestina  + Picha

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran siku zote imekuwa ikiwatetea na kuwaunga mkono raia wanaodhulimiwa na moja ya malengo muhimu ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ni kukombolewa Quds Tukufu na Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amebainisha wazi misimamo ya nchi hii kuhusu PalestIna na majukumu ziliyonayo nchi za Kiislamu katika kuwalinda na kuwatetea wananchi wa Palestina. Rais wa Iran aliyasema hayo jana alasiri katika kikao cha dharura cha Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) kilichofanyika mjini Istanbul, Uturuki na kuhudhuriwa na viongozi wa nchi zaidi ya 57 za Kiislamu.  

Akihutubia kikao hicho, Rais Rouhani amesisitiza kuundwa "Kundi la Wataalamu" litakalowajumuisha wataalamu wa masuala ya kisheria, kisiasa na kiuchumi kutoka nchi wanachama wa OIC kwa ajili ya kuchunguza kwa kina na kwa mapana katika ngazi za kimataifa, kieneo na kitaifa njia mbalimbali za kukabiliana na uamuzi ulio kinyume cha sheria uliochukuliwa hivi karibuni na serikali ya Marekani wa kuuhamishia katika mji wa Quds ubalozi wake wa Tel Aviv. Rais wa Iran aidha ametaka zichukuliwe hatua za kisiasa, kiuchumi na kibiashara dhidi ya serikali ya Marekani na utawala wa Kizayuni. 

AyatullahKhamenei akiwa katika mjumuiko wa maqari na wasomaji wa kaswida za Qur'ani  

Katika kadhia za hivi karibuni za Palestina na suala la Quds kuna nukta tatu muhimu zenye udharura wa kuzingatiwa  katika kuchambua suala hilo. 

Nukta ya kwanza ni  ukweli kuwa Wapalestina ndo wamiliki halali wa ardhi za Palestina na hakuna hatua mbadala wala utambulisho bandia unaoweza kubadilisha ukweli huu wa mambo. 

Nukta ya pili: ni hatua zisizo za kimantiki zilizochukuliwa katika siku za karibuni na kufuatia njama mpya za Washington na Tel Aviv; huku Wazayuni wakifanya jitihada za kutekeleza mpango wa kuikalia kwa mabavu kikamilifu Quds Tukufu chini ya mwavuli huo wa kuhamishiwa ubalozi wa Marekani huko Baitul Muqaddas.  

Nukta ya tatu: ni kutoweza kupindishika haki za wananchi wa Palestina. Wananchi hao hawajawahi kuwa tayari kufanya mazungumzo eti ya mapatano ili kuzikomboa ardhi zao kutoka kwenye makucha ya Wazayuni maghasibu; na kamwe hawatokaa katika meza eti ya mapatano na utawala wa Kizayuni. Leo hii pia wananchi wa Palestina wamejizatii zaidi na kusimama kidete kukabiliana na maghasibu wa Kizayuni japokuwa baadhi ya nchi za Kiarabu zimekuwa waitifaki wa utawala huo katika kuupa baraka ukaliaji huo wa mabavu. 

Akihutubia hivi majuzi mbele ya hadhara ya  maqari na wasomaji wa kaswida za Qur'ani, Ayatullah Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aliashiria matatizo na masaibu yanayoukumba Ulimwengu wa Kiislamu khususan hali waliyonayo wananchi wa Palestina na kueleza kuwa: Tumeshudia makumi ya Wapalestina wakiuliwa shahidi na maelfu ya wengine kujeruhiwa katika jinai za siku kadhaa za hivi karibuni za utawala khabithi na bandia wa Kizayuni; na katika mazingira hayo baadhi wanalalamika kuwa kwa nini Marekani haichukui hatua katika hali ambayo Marekani na serikali nyingi za Magharibi ni washirika wa jinai hizo.  

Abdul Bari Atwan, Mwandishi na mchambuzi mtajika katika Ulimwengu wa Kiarabu 

Abdul Bari Atwan mwandishi na mchambuzi mtajika katika Ulimwengu wa Kiarabu anasema kuhusiana na kuuliwa Wapalestina huko Ghaza kwamba: Hao walikuwa watu wasio na silaha ambao walipeperusha tu bendera zao na kuelekea mpakani. Kulikuwa na uzio mmoja tu wa mpakani baina ya raia hao na Waisraili. Waisraili walitumia silaha mbalimbali. Hata hivyo duru za habari za Kimagharibi zililieleza tukio hilo kuwa ni maandamano ya fujo. Je Wapalestina wanazo silaha? Je raia hao walikuwa na mada za mlipuko? Jambo hili halitasawariki. Hatua hiyo ya vyombo vya habari vya Magharibi ni sawa na kutoa taswira potofu kuhusu matukio yote. Vyombo hivyo vimeficha ukweli wa mambo.  

Ukweli wa mambo ni kuwa wananchi wa Palestina wanakabiliwa na dhulma kubwa ya kihistoria; na katika upande wa pili wa kadhia ya Palestina, kuna utawala ghasibu unaouwa watoto ambao kutokana na kuungwa mkono na Marekani umegeuka kuwa tatizo sugu kwa ulimwengu.

Katika mazingira kama hayo jamii ya kimataifa ukiwemo Ulimwengu wa Kiislamu, Umoja wa Mataifa na taasisi za kisheria za kimataifa zinawajibika na kubeba dhima ya kuwalinda na kuwatetea wananchi madhlumu wa Palestina; na pande zote hizo zinapaswa kutekeleza majukumu yao katika uwanja huo. 

Kwa ajili ya kukupa taswira japo ndogo kuhusu maandamano ya wananchi wa Palestina hapa chini tumekuwekea baadhi ya picha za maandamano hayo.