Kushadidi harakati za serikali ya Marekani dhidi ya Iran
https://parstoday.ir/sw/news/uncategorised-i37653-kushadidi_harakati_za_serikali_ya_marekani_dhidi_ya_iran
Serikali ya Marekani imeanzisha wimbi jipya la harakati za propaganda chafu dhidi ya Iran kwa tuhuma zisizo na msingi zilizotolewa na balozi wa nchi hiyoi katika Umoja wa Mataifa na miswada kadhaa iliyopasishwa na Kongresi ya nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 16, 2017 00:14 UTC
  • Kushadidi harakati za serikali ya Marekani dhidi ya Iran

Serikali ya Marekani imeanzisha wimbi jipya la harakati za propaganda chafu dhidi ya Iran kwa tuhuma zisizo na msingi zilizotolewa na balozi wa nchi hiyoi katika Umoja wa Mataifa na miswada kadhaa iliyopasishwa na Kongresi ya nchi hiyo.

Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Nikki Haley amedai katika matamshi yanayoshabihiana na mchezo wa kuigiza kwamba, Iran inawatumia silaha wapiganaji wa Yemen na kwamba kombora lililorushwa kuelekea Riyadh huko Saudi Arabia limetengenezwa nchini Iran. Haley amedai kuwa, Iran ni tishio kwa amani ya dunia na kwamba jamii ya kimataifa inapaswa kukabiliana na kile alichokiita "harakati zinazovuruga amani za Iran katika eneo la Mashariki ya Kati." 

Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Nikki Haley

Sambamba na hayo wawakilishi wa Kongresi ya Marekani wamepasisha miswada miwili dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Moja kati ya miswada hiyo unahusu kile kilichosemwa kuwa ni kuweka wazi mali za maafisa wa Iran, na mwingine umetaka kutolewe ripoti kuhusu mauzo ya ndege za abiria kwa Iran. 

Hatua hizo zimechukuliwa baada ya juhudi za Marekani za kutaka kuvuruga makubaliano ya nyuklia ya JCPOA kukumbana na kisiki kikubwa. Washington inatarajia kwamba, kwa kutumia wimbi jipya la propaganda chafu dhidi ya Iran na kuidhihirisha Jamhuri ya Kiislamu kuwa ni tishio, itafanikiwa kuunda muungano wa kikanda na kimataifa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu. Katika eneo la magharibi mwa Asia, Wamarekani wanategemea sana utawala wa kifalme wa Saudi Arabia na utawala haramu wa Isarel katika kile wanachosema ni "kuidhibiti Iran". Kwa sababu hiyo pia baada ya miaka mitatu ya kunyamazia kimya jinai na ukatili unaofanywa na Saudi Arabia dhidi ya watu wa Yemen, sasa Washington imeelekeza juhudi zake katika kile kinachosemwa kuwa ni misaada ya silaha ya Iran kwa wapiganaji wa al Huthi. Ili eti kuthibitisha madai hayo, Nikki Haley amejitokeza mbele ya vyombo vya habari akiwa na kipande alichodai kuwa, ni sehemu ya kombora lililorushwa Riyadh kutoka Yemen na kusema kina alama na nembo ya kiwanda cha Iran!

Nikki Haley

Madai hayo ya kuchekesha yametolewa baada ya kamati ya uchunguzi ya Umoja wa Mataifa kutangaza waziwazi kwamba, haiwezi kuthibitisha kuwepo mfungamano wowote baina ya Iran na kombora lililorushwa Riyadh na wapiganaji wa Yemen. 

Wakati huo huo Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Kudhibiti Silaha ya Marekani, Daryl Kimball amesema: "Matamshi yaliyotolewa na Nikki Haley akidai kuwa Iran imetuma kombora kwa wapiganaji wa Huthi wa Yemen yanakera na kuudhi."

Inastaajabisha kuona Marekani inazitaja harakati za Iran kuwa "zinavuruga amani na utulivu" ilhali rafiki na adui wanakiri kwamba, Tehran imekuwa na mchango mkubwa katika kuliangamiza kundi la kigaidi la Daesh katika nchi za Syria na Iraq. Itakumbukwa kuwa, katika siku ambazo magaidi wa Daesh walikuwa wakifanya mauaji na jinai za kutisha kwa msaada na himaya ya wazi na ya siri ya waitifaki wa Marekani kama Saudi Arabia, Imarati na Qatar, misaada ya Iran ndiyo iliyopelekea kulindwa miji mikubwa kama Baghdad na Damascus mbele ya hujuma za Daesh na kisha kusaidia kukombolewa miji kama Mosul, Aleppo, Raqqah na Deir al Zour kutoka kwenye makucha machafu ya magaidi hao.

Magaidi wa kundi la Daesh wakiuawa watu kwa umati Iraq na Syria

Hivi sasa ambapo baada ya kuangamizwa kundi la kigaidi la Daesh eneo la magharibi mwa Asia lina matarajio ya kurejea tena amani na utulivu, muungano wa Marekani, Saudi Arabia na Israel unafanya njama mpya ya kuwasha tena machafuko na vita katika eneo la Mashariki ya Kati na kuilenga Iran kwa aina mbalimbali ya hujuma za kipropaganda.