Kupasishwa mabaliko ya Katiba nchini Chad
https://parstoday.ir/sw/news/uncategorised-i43918-kupasishwa_mabaliko_ya_katiba_nchini_chad
Bunge la Chad limepasisha marekebisho ya Katiba ya nchi hiyo ambayo kivitendo yanampatia nguvu na mamlaka zaidi Rais Idriss Déby wa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 01, 2018 22:05 UTC
  • Kupasishwa mabaliko ya Katiba nchini Chad

Bunge la Chad limepasisha marekebisho ya Katiba ya nchi hiyo ambayo kivitendo yanampatia nguvu na mamlaka zaidi Rais Idriss Déby wa nchi hiyo.

Kwa mujibu wa marekebisho hayo ya Katiba, muhula wa Rais utaongezwa kutoka miaka 5 na kuwa miaka 6, huku kipindi cha Ubunge nacho kikiongezwa kutoka miaka minne na kuwa mitano. Aidha kwa mujibu wa mabadiliko hayo, cheo cha Waziri Mkuu kimefutwa huku taasisi kama Baraza la Katiba na Mahakama ya Ukaguzi wa Mahesabu zikiunganishwa na kujumuishwa na Mahakama Kuu. Marekebisho hayo ya Katiba hasa ya kufuta cheo cha Waziri Mkuu kivitendo yanamuongezea nguvu na mamlaka Rais Idriss Deby wa nchi hiyo. Aidha kwa mujibu wa marekebisho hayo, Rais Deby ataruhusiwa kugombea tena katika uchaguzi ujao wa Rais.

Marekebisho ya Katiba yamepasishwa na Bunge la Chad katika hali ambayo, wapinzani na makundi ya kiraia nchini humo yanalalamikia vikali marekebisho hayo. Kwa mtazamo wa wapinzani ni kuwa, mpango huo hauna uhalali wa kisheria. Katika uwanja huo, vyama vyote vya upinzani hivi karibuni vilisaini taarifa rasmi ya kuupinga mpango huo wa kufanyia marekebisho Katiba ya nchi hiyo. Kanisa Katoliki nchini Chad na Baraza la Sheria la nchi hiyo ni miongoni mwa wapinzani wa marekebisho hayo.

Hali ya maisha ni mbaya katika baadhi ya maeneo ya Chad

Wanaopinga marekebisho hayo wanasema kuwa, uamuzi kuhusiana na Katiba ya nchi kikiwa chombo cha kuaminika cha kijamii haupaswi kuachiwa Bunge pekee. Baraza la Sheria la Chad likitegemea sheria limetangaza msimamo wake na kutaka kufanyika kura ya maoni kwa ajili ya kufanyia mabadiliko Katiba. Marekebisho ya Katiba nchini Chad yamefanyika katika hali ambayo, kabla ya hapo pia yaani mwaka 2005, Katiba ya nchi hiyo ilifanyiwa marekebisho ambapo kwa mujibu wa marekebisho hayo, ukomo wa Rais kuongoza kwa mihula miwili tu uliondolewa.

Wapinzani wanasema kuwa, mabadiliko hayo yanamuandalia uwanja Rais Idriss Deby kuendelea kubakia madarakani. Rais Deby amekuwa madarakani tangu mwaka 1990 baada ya kuondolewa uongozini dikteta wa zamani wa nchi hiyo Hissène Habré. Aidha wanaopinga marekebisho hayo wanaamini kwamba, kuendelea kubakia madarakani Rais Idriss Deby ni kinyume na mchakato wa demokrasia na kunaipeleka nchi hiyo upande wa kuanzisha udikteta katika nchi hiyo ya Kiafrika. Hasa kwa kutilia maanani kwamba, katika miaka ya hivi karibuni baadhi ya viongozi wa Kiafrika kama Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi na Paul Kagame wa Rwanda wamezifanyia marekebisho Katiba za nchi zao na hivyo kujiandalia uwanja wa kuendelea kubakia madarakani.

Wanajeshi wa Chad wakiwa katika operesheni ya kuwasaka wapiganaji wa Boko Haram

Anga hiyo ya kisiasa nchini Chad inatawala katika hali ambayo, nchi hiyo filihali inakabiliwa na migogoro  tofauti. Ukosefu wa usalama unaosababishwa na harakati za kundi la kigaidi la Boko Haram katika Ukanda wa Ziwa Chad, kuongezeka idadi ya wakimbizi, kuporomoka bei ya mafuta katika soko la dunia na kuongezeka gharama za kijeshi na kiusalama ni mambo ambayo yameifanya nchi hiyo ikabiliwe na matatizo ya kiuchumi, umasikini na ukosefu wa ajira.

Ili kukabiliana na matatizo hayo, serikali ya Chad iliamua kutekeleza mpango wa kubana matumizi, sera ambayo nayo ilipelekea kuongezeka malalamiko ya wananchi. Edmond Goetbé Djitangar, Askofu Mkuu wa N'Djamena mji mkuu wa Chad sambamba na kutahadharisha kuhusiana na hali inayotawala hivi sasa katika nchi hiyo amesema kuwa, Chad inakabiliwa na mgogoro wa kijamii usio na kikomo na ambao utawafanya wananchi kukabiliwa na matatizo mengi.

Hivi sasa licha ya kuweko matatizo ya kiuchumi na kisiasa nchini Chad, inaonekana kuwa, marekebisho ya Katiba ni jambo jingine ambalo litaongeza wigo wa malalamiko na matakwa ya wananchi wa nchi hiyo.