Bahrain; uwanja wa maandamano makubwa dhidi ya utawala wa Aal Khalifa
https://parstoday.ir/sw/news/uncategorised-i47084-bahrain_uwanja_wa_maandamano_makubwa_dhidi_ya_utawala_wa_aal_khalifa
Maelfu ya watu katika eneo la Diraz nchini Bahrain ambalo ndipo yalipo makazi ya Sheikh Issa Qassim, mwanazuoni mtajika wa nchi hiyo wamefanya maandamano makubwa; na huku wakiwa wamebeba picha za alimu huyo ambaye kwa sasa yupo nje ya nchi kwa matibabu wamepiga nara dhidi ya sera za mfumo unaotawala nchini humo ambao umekuwa ukikanyaga haki za maulama na wapinzani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 28, 2018 20:52 UTC
  • Bahrain; uwanja wa maandamano makubwa dhidi ya utawala wa Aal Khalifa

Maelfu ya watu katika eneo la Diraz nchini Bahrain ambalo ndipo yalipo makazi ya Sheikh Issa Qassim, mwanazuoni mtajika wa nchi hiyo wamefanya maandamano makubwa; na huku wakiwa wamebeba picha za alimu huyo ambaye kwa sasa yupo nje ya nchi kwa matibabu wamepiga nara dhidi ya sera za mfumo unaotawala nchini humo ambao umekuwa ukikanyaga haki za maulama na wapinzani.

Tangu mwaka 2011, Bahrain imekuwa ikishuhudia wimbi la malalamiko makubwa ya wananchi wa nchi hiyo ambao wanataka kuondoka madarakani utawala wa kifamilia wa Aal Khalifa na kuachiliwa huru wafungwa wa kisiasa wanaoshikiliwa katika magereza ya nchi hiyo. Kuendelea maandamano dhidi ya utawala wa Bahrain katika mwaka huu wa 2018 ni bainisho la wazi la azma thabiti ya wananchi wa nchi hiyo ya kuendeleza harakati yao dhidi ya utawala wa kidikteta wa Aal Khalifa.

Kuchukua wigo mpana harakati za malalamiko na maandamano ya amani ya wananchi hao mkabala na ukandamizaji wa utawala wa Aal Khalifa unaofanyika kwa aina tofauti kumeufanya utawala huo uchanganyikiwe na kushindwa kufikia malengo yake ya  kusambaratisha harakati ya wananchi hao. Kwa mujibu wa vyanzo vya asasi za haki za binadamu, Bahrain ikiwa nchi ndogo zaidi miongoni mwa nchi za Kiarabu za Magharibi mwa Asia ina wafungwa wengi zaidi wa kisiasa.

Maandamano ya wananchi wa Bahrain

Vitendo vya ukandamizaji na vya utumiaji mabavu vya utawala wa Aal Khalifa dhidi ya wapinzani vimewafanya walimwengu, zikiwemo asasi za haki za binadamu, kuingiwa na wasiwasi mkubwa kuhusiana na hali, hatima pamoja na majaaliwa ya wanaharakati wa kisiasa na wapinzani wa utawala huo. Kuzorota hali ya kiafya ya Sheikh Issa Qassim ni dhihirisho la muamala wa kidhalimu wa mfumo unaotawala nchini Bahrain dhidi ya wapinzani. Sheikh Issa Qassim ni mwanazuoni mtajika wa Bahrain ambaye baada ya miaka miwili ya kuzingirwa makazi yake na vikosi vya usalama, takribani wiki tatu zilizopita  alipelekwa mjini London Uingereza  kwa ajili ya matibabu.

Takribani miaka miwili iliyopita, utawala wa Bahrain ulimpokonya uraia alimu huyo na kuyazingira makazi yake katika eneo la Diraz na kwa msingi huo akawa amewekwa katika kifungo cha nyumbani. Ni kuanzia kipindi hicho na baada yake ndipo hali ya kiafya ya Sheikh Issa Qassim ilipozorota na kuzidi kuwa mbaya siku baada ya siku. Licha ya malalamiko na wasiwasi wa jamii ya kimataifa, utawala wa Aal Khalifa unaopata uungaji mkono wa madola ya Magharibi umekuwa ukipuuza ukosoaji unaoongezeka dhidi yake wa asasi za haki za binadamu kwa siasa zake za kipolisi dhidi ya wapinzani, na kuendelea kuwapokonya raia wa nchi hiyo haki za awali kabisa za kibinadamu.

Katika ripoti yake ya hivi karibuni kwa ofisi ya Haki ya za Binadamu ya Umoja  wa Mataifa huko Geneva Uswisi, Kamati ya Kimataifa ya Haki za Binadamu ilielezea wasiwasi ilionao kuhusiana na hali ya haki za binadamu nchini Bahrain na kusema kuwa, hali ya wapinzani katika nchi hiyo ya Kiarabu ya Ghuba ya Uajemi imekuwa mbaya zaidi ikilinganishwa na mwaka jana. Ripoti hiyo inasisitiza kuwa, uhuru wa kutoa maoni umebinywa zaidi  na marekebisho ya Katiba ambayo yanatoa idhini ya kushtakiwa na kuhukumiwa wanaharakati wa kiraia katika mahakama za kijeshi nayo yameifanya hali ya mambo izidi kuwa mbaya. 

Sheikh Issa Qassim, mwanazuoni mtajika wa Bahrain ambaye amekuwa akiandamwa na utawala wa Aal Khalifa

Utawala wa Bahrain umekuwa ukitumia kila wenzo kama tuhuma zisizo na msingi na mbinu za kidhalimu ili kuwaandama wanaharakati wa kisiasa ambao kimsingi takwa lao ni kuweko nchini humo utawala wenye ridhaa ya wananchi na kuheshimiwa haki za watu. Kwa hatua kama hizo utawala huo unataka kuzusha woga na wahaka miongoni mwa wanaharakati wa kisiasa nchini Bahrain ili kwa njia hiyo uyakandamize malalamiko ya wananchi ambayo yamekuwa yakishadidi kila siku tangu yalipoanza mwaka 2011. Fauka ya hayo, utawala huo umewanyima wananchi haki mbalimbali kama uhuru wa kutoa maoni, mikusanyiko ya amani na kuunda vyama na makundi ya kisiasa. 

Ripoti mbalimbali kutoka nchini Bahrain zinaonyesha kuwa, ukiukaji wa haki za binadamu ambao umekuwa ukifanywa na utawala wa Aal Khalifa na ambao unajumuisha utiaji mbaroni wa kidhulma, kuvamia majumba, kuwafungulia mashtaka kidhulma raia, kukandamiza maandamano ya amani na kupokonya uraia umeshadidi mno nchini humo. Lengo la siasa za watawala wa Bahrain ni kushadidisha anga ya mbinyo nchini humo suala ambalo limezifanya fikra za waliowengi ulimwenguni kuingiwa na wasiwasi mkubwa. Bila shaka kuenea ripoti mbalimbali kuhusiana na mazingira mabaya ya wanaharakati wa kisiasa nchini Bahrain ni jambo linaloakisi wasiwasi huo.