Apr 10, 2016 07:51 UTC
  • Idadi ya waliokufa katika mkasa wa moto India yapindukia 100

Idadi ya watu waliopoteza maisha katika mkasa wa moto uliotokea alfajiri ya leo kusini mwa India imepindukia 100.

Polisi ya India imethibitisha kuwa watu zaidi ya 102 wameaga dunia na wengine zaidi ya 200 kujeruhiwa katika mkasa huo unaohesabika kuwa mkubwa katika miezi ya hivi karibuni, uliotokea mapema leo katika mji wa bandari wa Kollam, kusini mwa India.

Habari zinasema kuwa, moto huo uliotokea katika Hekalu la Puttingal katika kitongoji cha Paravur jimbo la Kerala, ulisababishwa na kuripuliwa mafataki, wakati wa maandalizi ya sherehe za Vishu, za kuadhimisha mwaka mpya wa jamii ya Wahindu. Sherehe hizo zinazojulikana kama ‘Hafla za Mwanga na Fataki’ zinatazamiwa kufanyika Aprili 14.

Waziri wa Masuala ya Ndani wa jimbo la Kerala, Ramesh Chennitah amethibitisha kutokea mkasa huo na ameagiza maafisa usalama kushirikiana na timu za waokoaji ili kuokoa manusura na kuwapeleka hospitalini.

Vyombo vya habari vya India vimeripoti kuwa, kwa sasa moto huo umedhibitiwa na manusura wamekimbizwa katika hospitali ya mji wa Thiruvananthapuram, makao makuu ya jimbo hilo.

Itakumbukwa kuwa, tarehe Mosi Januari mwaka huu, watu kadhaa waliaga dunia katika mkasa mwingine wa moto wa kukaribisha mwaka mpya mjini Dubai, katika Umoja wa Falme za Kiarabu. Moto huo ulizuka baada ya kuripuliwa mafataki ya kuukaribisha mwaka mpya kwenye Hoteli ya Adress Downtown yenye ghorofa 63 na iliyoko karibu na jengo refu zaidi duniani la Burj al-Khalifa.

Tags