Pango la Simba: Tutafanya operesheni nyingi zaidi dhidi ya Israel
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i100454-pango_la_simba_tutafanya_operesheni_nyingi_zaidi_dhidi_ya_israel
Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina ya Arin al Usud (Pango la Simba) imeuonya utawala wa Kizayuni wa Israel kwamba ujiandae kupokea vipigo vikali zaidi kutoka kundi hilo la mapambano.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 29, 2023 06:43 UTC
  • Pango la Simba: Tutafanya operesheni nyingi zaidi dhidi ya Israel

Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina ya Arin al Usud (Pango la Simba) imeuonya utawala wa Kizayuni wa Israel kwamba ujiandae kupokea vipigo vikali zaidi kutoka kundi hilo la mapambano.

Taarifa ya Arin al Usud imesema, harakati hiyo itafanya operesheni nyingi zaidi dhidi ya Wazayuni, huku ikitoa mwito wa umoja na kushirikiana makundi ya muqawama ya Palestina.

Imesema itaelekeza mashambulizi zaidi dhidi ya utawala haramu wa Israel katika eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, ikisisitiza kuwa maadui hawaelewi lugha nyingine isipokuwa lugha ya 'damu na upanga'.

Kundi hilo la muqawama limeapa kulipiza kisasi cha mauaji ya kikatili ya Wapalestina katika eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Taarifa ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina ya Arin al Usud imekuja wakati huu ambapo vikosi vya utawala pandikizi wa Israel vimeshadidisha ukatili wao dhidi ya Wapalestina wa Ukingo wa Magharibi.

Askari wa KIzayuni wanavyowakandamiza Wapalestina Ukingo wa Magharibi

Mapema jana Ijumaa, Wapalestina kadhaa walijeruhiwa kwa kupigwa risasi na wanajeshi wa utawala katili wa Israel katika kijiji cha Kafr Qaddum, kaskazini mwa mkoa wa Qalqilia katika eneo la Ukingo wa Magharibi.

Aidha juzi Alkhamisi, Itamar Ben-Gvir, Waziri wa Usalama wa Ndani wa utawala wa Kizayuni aliongoza kundi la walowezi wa Kizayuni kuushambulia Msikiti wa al Aqsa, wakitokea upande wa  Bab al Magharib.