Brigedia Jenerali Jazayeri: Saudia haina haki ya kuingilia mambo ya Iraq
Afisa mwandamizi wa jeshi la Iran amesema Saudi Arabia na watawala wake hawana haki ya kuingilia mambo ya ndani ya Iraq na kwamba wanapaswa kuheshimu matakwa ya Wairaqi.
Brigedia Jenerali Massoud Jazayeri ambaye ni naibu Mkuu wa Majeshi ya Iran ametahadharisha kuhusu njama za Marekani na washirika wake za kutaka kuisambaratisha Iraq na Syria na kusema: "Nyaraka na ushahidi uliopo unaonesha kwamba Marekani inataka kudhoofisha nchi za Kiislamu."
Amesema Marekani na Wazayuni wameanzisha vita vinavyopiganwa kwa niaba yao katika eneo la Mashariki ya Kati.
Brigedia Jenerali Jazayeri ametahadharisha kuwa Marekani inataka kuchochea vita na mikwaruzano kati ya Waislamu wa madhehebu za Shia na Suni kwa shabaha ya kutimiza malengo yake na kudhamini usalama wa Israel.
Vilevile amelipongeza jeshi na wananchi wa Iraq kwa kukomboa mji wa kistratijia wa Fallujah kutoka kwenye makucha ya kundi la kigaidi la Daesh.
Jana Jumapili kamanda anayeongoza operesheni ya kukomboa mji huo alitangaza kuwa umekombolewa kikamilifu. Luteni Jenerali Abdul Wahab al-Saidi amesema kuwa magaidi 1,800 wa kundi hilo la kitakfiri wameuawa katika operesheni hiyo.
Mji wa Fallujah ilioko umbali wa kilomita 65 magharibi mwa Baghdad ulikuwa wa kwanza kutekwa na wapiganaji wa kundi la kigaidi la Daesh Januari mwaka 2014.