Iran, Saudia zaafikiana kuimarisha usalama na ustawi wa Asia Magharibi
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i101224-iran_saudia_zaafikiana_kuimarisha_usalama_na_ustawi_wa_asia_magharibi
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Hossein Amir-Abdollahian amekutana na kufanya mazungumzo mjini Jeddah na Mohammed bin Salman, Mrithi wa Ufalme wa Saudi Arabia, ambapo wametilia mkazo wajibu wa kustawishwa zaidi uhusiano wa kiusalama na maendeleo ya nchi mbili hizi na eneo zima la Asia Magharibi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 19, 2023 00:23 UTC
  • Iran, Saudia zaafikiana kuimarisha usalama na ustawi wa Asia Magharibi

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Hossein Amir-Abdollahian amekutana na kufanya mazungumzo mjini Jeddah na Mohammed bin Salman, Mrithi wa Ufalme wa Saudi Arabia, ambapo wametilia mkazo wajibu wa kustawishwa zaidi uhusiano wa kiusalama na maendeleo ya nchi mbili hizi na eneo zima la Asia Magharibi.

Amir-Abdollahian alibainisha hayo katika ujumbe alioutuma kwenye mtandao wa kijamii wa X (Twitter) jana Ijumaa ambapo amesisitiza kuwa, amefanya mazungumzo ya kina, ya wazi na yaliyozaa matunda kwa takriban dakika 90 mjini Jeddah na Bin Salman. 

Amesema Iran na Saudia zimeafikiana kuimarisha uhusiano na ushirikiano wao endelevu katika nyuga mbali mbali, kwa misingi ya sera ya ujirani mwema.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitiza kwamba, Jamhuri ya Kiislamu na Saudi Arabia ni nchi mbili muhimu katika eneo la Asia Magharibi. 

"Tumekubaliana juu ya usalama na ustawi kwa ajili ya wote katika eneo", ameeleza mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwenye ujumbe wake huo kwenye mtandao wa X, ambao huko nyuma ulikuwa unafahamika kama Twitter.

Amir-Abdollahian amesema, uhusiano wa nchi hizi mbili uko kwenye mkondo sahihi hivi sasa na unazidi kunawiri na kwamba Tehran na Riyadh zinatilia mkazo udharura wa kutekelezwa vipengee vyote vya maafikiano yaliyotiwa saini na pande mbili katika masuala ya uchumi, biashara na usalama.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Alkhamisi alipokutana na mwenzake wa Saudia, Faisal bin Farhan

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran juzi Alkhamisi alikutana na mwenzake wa Saudia, Faisal bin Farhan na kubainisha kuwa, Jamhuri ya Kiislamu na Saudi Arabia zinabeba jukumu zito la kihistoria mkabala wa ustawi na maendeleo ya dunia.

Nchi mbili za Iran na Saudia zilirejesha uhusiano wao tarehe 10 Machi 2023 kwa upatanishi wa China, baada ya kupita miaka 7 ya Saudia kuvunja uhusiano wake wa kidiplomasia na Jamhuri ya Kiislamu.