Balozi wa Saudia awasili Tehran; wa Iran pia akaribishwa Riyadh
Baada ya kupita miaka kadhaa tangu kuvunjika uhusiano wa kidiplomasia baina ya Iran na Saudi Arabia, Balozi mpya wa Saudia amewasili hapa Tehran; hatua inayoashiria kufunguliwa kwa ukurasa mpya wa uhusiano baina ya mataifa haya mawili.
Shirika la habari la Iran Press limeripoti habari hiyo na kueleza kuwa, Abdullah bin Saud al-Anzi , Balozi wa Saudi Arabia aliwasili hapa mjini Tehran jana Jumanne na kupokewa na maafisa wa ngazi za juu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Shirika la habari la Saudia (SPA) limemnukuu Balozi al-Anzi akisema mara baada ya kuwasili hapa Tehran kuwa: Miongozo ya uongozi wa Saudia inasisitiza juu ya kuimarisha mahusiano, mawasiliano na mikutano baina ya ufalme (wa Saudia) na Iran katika nyuga tofauti.
Amesema kuhuishwa uhusiano uliokuwa umevunjika kwa miaka saba baina ya Iran na Saudia kutaimarisha ushirikiano na kuyanufaisha mataifa haya mawili, mbali na kujenga hali kuaminiana baina yao.
Jana Jumanne pia, Alireza Enayati, Balozi mpya wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Saudi Arabia aliwasili Riyadh na kupokewa na maafisa wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Saudia.
Kabla ya kuondoka nchini, Balozi Enayati alikutana na Rais Sayyid Ebrahim Raisi kwa ajili ya kupewa miongozo na nasaha za mwisho kabla ya kuelekea Riyadh kuiwakilisha Jamhuri ya Kiislamu kama balozi kamili wa Iran.
Katika mazungumzo hayo, Sayyid Raisi alisema kustawi na kuongezeka ushirikiano wa nchi za ukanda huu kutaziinua nchi hizo katika milingano ya kimataifa, na kwamba kuna wajibu wa kuimarishwa ushirikiano wa pande zote wa nchi za eneo hili.
Rais wa Iran alisema: Ushirikiano wa Iran na Saudi Arabia na kuongezeka ushirikiano wa nchi za eneo eneo hili katika nyuga tofauti za baina ya pande mbili na pande kadhaa na katika masuala ya Ulimwengu wa Kiislamu kiujumla, kutaimarisha nafasi ya nchi za eneo hili kwenye milingano ya kikanda na kimataifa na kuzuia uingiliaji wa madola ajnabi katika masuala ya nchi hizo.