Kushtadi mvutano kati ya Netanyahu na Biden kuhusu Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i106734-kushtadi_mvutano_kati_ya_netanyahu_na_biden_kuhusu_gaza
Gazeti la Marekani la New York Times limetangaza katika ripoti iliyowanukuu maafisa wa Marekani na Wazayuni kwamba, mazungumzo ya hivi karibuni kati ya Rais Joe Biden wa Marekani na Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel yalitawaliwa na malumbano na kurushiana maneno.
(last modified 2024-01-02T23:16:59+00:00 )
Jan 02, 2024 23:16 UTC
  • Kushtadi mvutano kati ya Netanyahu na Biden kuhusu Gaza

Gazeti la Marekani la New York Times limetangaza katika ripoti iliyowanukuu maafisa wa Marekani na Wazayuni kwamba, mazungumzo ya hivi karibuni kati ya Rais Joe Biden wa Marekani na Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel yalitawaliwa na malumbano na kurushiana maneno.

Licha ya kuwa, Marekani inatoa himaya na uungaji mkono kamili kwa utawala wa Kizayuni katika vita dhidi ya Gaza, lakini kuna tofauti na hitilafu za kimtazamo kati ya pande hizo. Mzozo na mvutano mkubwa zaidi baina ya pande hizo mbili ni kuhusu uendeshaji na usimamizi wa Gaza baada ya kumalizika kwa vita. Marekani inapinga kuendelea kukaliwa kwa mabavu Gaza baada ya kumalizika vita vya ardhini vya utawala wa Kizayuni, lakini baraza la mawaziri la Netanyahu linasisitiza juu ya mipango ya usalama pamoja na kuwepo askari na jeshi huko Gaza hata baada ya kumalizika vita hivyo.

Tofauti nyingine muhimu ni kuhusiana na mbinu za vita za utawala wa Kizayuni. Rais Joe Biden wa Marekani amemwambia Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni Benjamin Netanyahu kwamba, Israel inapoteza uungwaji mkono wa kimataifa kutokana na mashambulizi ya kiholela dhidi ya Gaza na kwamba Netanyahu anapaswa kubadilisha serikali yake ambayo inaongozwa na vyama vya siasa vya mrengo wa kulia vyenye misimamo ya kufurutu ada na kukomesha mashambulizi hayo ambayo yanasababisha mauaji ya halaiki na badala yake ifanye mashambulio ya mabomu dhidi ya Harakati ya HAMAS. Netanyahu amepuuzilia mbali maonyo na indhari za Ikulu ya White House, na anadai kusonga mbele huko Gaza hadi atakapolisambaratisha eneo hilo na kusema kwamba vita hivi vitadumu kwa miezi kadhaa.

Wapalestiina zaidi ya 22,0000 wameuawa shahidi tangu Israel ilipoanzisha hujuma na mashambulio ya kinyama huko Gaza Oktoba mwaka jana (2023)

 

Nukta ya tatu ni kwamba, Joe Biden ana wasi wasi kuhusu matokeo ya vita vya Gaza na uungaji mkono usio na shaka kwa utawala wa Kizayuni katika medani ya kisiasa ya Marekani. Uchaguzi wa rais wa Marekani umepangwa kufanyika mwaka huu (2024) na kuna uwezekano Joe Biden akachuana tena na Donald Trump, mpinzani kutoka chama cha Republican na rais wa zamani wa Marekani. Joe Biden anaamini kuwa vita vya Gaza vitaathiri uchaguzi wa Marekani na Netanyahu pia anataka Warepublican kupata mamlaka.

Kwa muktadha huo, ingawa utawala wa Biden unatoa himaya na uungaji mkono wa kila upande kwa utawala wa Kizayuni katika vita dhidi ya Gaza, ikiwa ni pamoja na kwamba hadi sasa umepiga kura ya turufu kuzuia maazimio kadhaa ya kutaka kusitishwa mara moja vita huko Gaza, lakini rais wa Marekani alimwambia Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel kwamba, hana imani naye.

Maandamano ya Wamarekani dhidi ya sera za Rais Biden wa Marekani

 

Nukta ya nne ni kwamba, Biden na baraza lake la mawaziri wanaamini kuwa, hadi sasa vita vya Gaza na mbinu za kivita za Israel zimewagharimu kwa sababu vimesababisha kuanzishwa maandamano ya kimataifa dhidi ya Marekani kutokana na uungaji mkono wake kamili na usio na masharti kwa Tel Aviv. Kwa hakika, uungaji mkono wa pande zote wa Marekani kwa utawala wa Kizayuni katika vita dhidi ya Gaza umeifanya serikali ya Marekani kupoteza hadhi, heshima na kupuuzwa kikamilifu na fikra za waliowengi uimwenguni.

Kwa upande mmoja, serikali ya Marekani inaunga mkono mauaji ya kimbari dhidi ya wakazi wa Gaza yanayofanywa na wavamizi wa Kizayuni, na kwa upande mwingine inadai kuunga mkono haki za binadamu. Vita vya Gaza vimefichua na kuweka wazi zaidi sura halisi ya Marekani mbele ya walimwengu na hilo limemfanya Biden na serikali yake kutofurahishwa na jambo hilo.