Jeshi la Yemen lashambulia meli nyingine ya US Ghuba ya Aden
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i107410-jeshi_la_yemen_lashambulia_meli_nyingine_ya_us_ghuba_ya_aden
Msemaji wa Jeshi la Yemen amesema vikosi vya ulinzi vya nchi hiyo vimeshambulia meli nyingine ya Marekani iliyokuwa ikipita katika Ghuba ya Aden.
(last modified 2024-01-20T00:33:06+00:00 )
Jan 20, 2024 00:33 UTC
  • Jeshi la Yemen lashambulia meli nyingine ya US Ghuba ya Aden

Msemaji wa Jeshi la Yemen amesema vikosi vya ulinzi vya nchi hiyo vimeshambulia meli nyingine ya Marekani iliyokuwa ikipita katika Ghuba ya Aden.

Brigedia Jenerali Yahya Saree, Msemaji wa Jeshi la Yemen alinukuliwa akisema hayo jana Ijumaa na kanali ya televisheni ya Al-Masirah na kuongeza kuwa, vikosi vya nchi hiyo ya Kiarabu vimelenga na kuishambulia kwa makombora ya baharini meli ya kibiashara ya Marekani ya Chem Ranger, katika Ghuba ya Aden.

Saree ameeleza bayana kuwa, meli nyingine zote isipokuwa za Marekani, Uingereza na Israel zipo salama kupita katika maji ya Bahari Nyekundu na kusisitiza kuwa, hazitalengwa na kushambuliwa na vikosi vya Yemen.

Msemaji wa Jeshi wa la Yemen amebainisha kuwa, vikosi vya Yemen vitaendelea kujibu uvamizi na uchokozi wa Marekani na Uingereza dhidi ya Yemen kupitia mashambulizi ya ardhini na baharini.

Hali ya usalama katika Bahari Nyekundu imezidi kuwa mbaya kufuatia mashambulizi ya Marekani na Uingereza dhidi ya Wayemen katika siku za hivi karibuni.

Ghuba ya Aden

Makampuni kadhaa ya meli duniani, ikiwa ni pamoja na makampuni yanayoongoza katika sekta ya nishati, yameelekeza meli zao kwenye njia ndefu na ya gharama kubwa zaidi kuzunguka Rasi ya Tumaini Jema (Cape of Good Hope) ya Afrika Kusini kwa hofu ya kushambuliwa wakati zinapovuka Bahari ya Sham.

Viongozi wa Yemen wanasema kuwa, wameamua kuzuia meli zinazoelekea kwenye bandari za Israel ili kuulazimisha utawala wa Kizayuni ukomeshe jinai zao dhidi ya Wapalestina hasa wa Ukanda wa Gaza. Lakini Marekani na Uingereza zimeanzisha vita dhidi ya Yemen kuunga mkono jinai za Israel badala ya kuushinikiza utawala wa Kizayuni ukomeshe jinai hizo.