Vita vya Gaza na kuongezeka changamoto ndani ya utawala wa Kizayuni
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i107428-vita_vya_gaza_na_kuongezeka_changamoto_ndani_ya_utawala_wa_kizayuni
Kuendelea vita vya utawala haramu wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza kumezidisha changamoto ndani ya utawala huo ghasibu.
(last modified 2026-05-04T12:51:55+00:00 )
Jan 20, 2024 04:45 UTC
  • Vita vya Gaza na kuongezeka changamoto ndani ya utawala wa Kizayuni

Kuendelea vita vya utawala haramu wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza kumezidisha changamoto ndani ya utawala huo ghasibu.

Siku 106 zimepita tangu vilipoanza vita vya utawala wa Kizayuni dhidi ya Ukanda wa Gaza. Hadi sasa vita hivyo vimesababisha maafa mengi na makubwa kwa Wapalestina, lakini hata utawala wa Kizayuni pia umepata hasara kadhaa kutokana na vita hivyo. Miongoni mwa hasara hizo ni za kiuchumi, kijamii na kisiasa.
Kwa upande wa kiuchumi, siku 106 za vita zimeutia hasara kubwa utawala wa Kizayuni. Katika ripoti yake mpya, gazeti la Economist limeandika yafuatayo kuhusu athari za vita vya Gaza kwa uchumi wa Israel: "athari mbaya na haribifu za vita hivi zitaendelea kuiyumbisha hali ya kiulinzi na kiuchumi ya utawala wa Israel kwa miaka mingi ijayo".

Gazeti hilo limeendelea kueleza katika ripoti yake hiyo kwamba: "gharama kubwa za kiuchumi za vita vya Gaza, sio tu zilifikia dola bilioni nne na milioni mia tano katika mwezi Desemba-ikiwa ni sawa na asilimia moja ya Pato la Taifa-lakini pia zimepelekea kupungua kwa 8% mapato ya kodi katika mwaka 2023".

Nukta nyingine muhimu kwa mtazamo wa kiuchumi ni kwamba, athari za vita hivyo hazihusiani na kipindi cha vita pekee, lakini katika mwaka huu wa 2024 na itakayofuatia, zitakuwa na taathira nyingi hasi kwa uchumi wa utawala huo.
Gazeti la Economist limeandika, "uchumi wa utawala wa Israel utalazimika kufidia kwa miaka na miaka gharama za vita hata baada ya kumalizika vita hivi".
Benki ya JP Morgan Chase hivi karibuni iliandika katika ripoti yake kuwa: "ukubwa wa uchumi wa Israel utapungua kwa 11% katika robo ya mwisho ya mwaka huu (2024) kutokana na vita vya Gaza".
Mara ya mwisho kushuhudiwa kupungua kwa uchumi wa utawala wa Kizayuni wa Israel ilikuwa ni katika mwaka 2020 baada ya msambao wa kirusi cha Corona.
Baadhi ya chambuzi zinaonyesha kuwa, athari za vita vya Gaza kwa uchumi wa utawala ghasibu wa Israel zitakuwa kubwa zaidi kuliko taathira hasi zilizosababishwa na kirusi cha corona kwa uchumi wa utawala huo.

Kwa upande wa kijamii, ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu zilizopachikwa jina bandia la Israel zinashuhudia maandamano ya familia za mateka wa Kizayuni dhidi ya baraza la mawaziri la Benjamin Netanyahu.

Siku ya Alkhamisi ya tarehe 18 Januari, familia hizo za mateka wa Kizayuni zilifunga barabara kuu ya Ayalon mjini Tel Aviv ikiwa ni ishara ya kulalamikia kutoshughulikiwa kadhia ya mateka wao.
Baraza la Mawaziri la Netanyahu limeamua kutumia njia moja tu kwa ajili ya kuwakomboa mateka wa Kizayuni, nayo ni kuendeleza vita dhidi ya Gaza.
Hii ni pamoja na ukweli kwamba, katika muda wa siku 106 zilizopita, ni mateka 70 pekee wa Kizayuni walioachiwa huru; na kuachiwa kwao hakukufanikishwa kwa nguvu za vita.
Kwa hakika utawala wa Kizayuni haukuweza kuwapata mateka wake kwa njia ya vita, bali ulilazimika kusitisha vita kwa muda wa siku saba, na ndani ya muda huo ndipo mateka wake 70 wakaachiwa huru.
Hivi sasa baraza la mawaziri la vita la Israel linajaribu kutumia kila mbinu za kivita ili kuwakomboa mateka wake, wakati haljafanikiwa kupatambua hata mahali walipowekwa mateka hao.
Ni kwa sababu hii, ndipo familia za mateka hao zikaamua kuandamana ili kubainisha wasiwasi zilionao kuhusu afya za mateka wao na kutoridhishwa kwao na utendaji wa baraza la mawaziri la Netanyahu.

Ama kwa upande wa kisiasa, mbali na kuongezeka mpasuko uliopo kati ya wananchi na baraza la mawaziri la Netanyahu, miito na mashinikizo ya wananchi hao pamoja na wakosoaji ya kumtaka waziri mkuu huyo ang'atuke madarakani yameongezeka pia.

Kutokana na vita vya Gaza, baraza la mawaziri la Netanyahu liko katika hali tete zaidi kuwahi kushuhudiwa katika kipindi cha mwaka mmoja sasa.../