HAMAS: 'Tunapitia' pendekezo jipya la kusimamisha vita Gaza
Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amesema kundi hilo la muqawama 'linadurusu' na kutathmini pendekezo jipya la usitishaji vita lakini amesisitiza kuwa, kipaumbele chake kwa sasa ni kuhitimisha uvamizi na kuondoka kikamilifu vikosi vamizi vya utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ukanda wa Gaza.
Ismail Haniya alisema hayo jana Jumanne katika taarifa na kuongeza kuwa, HAMAS inapitia pendekezo la usitishaji mapigano lililowasilishwa na maafisa wa Qatar na Misri katika mikutano ya karibuni nchini Ufaransa, na kwamba karibuni harakati hiyo itatoa jibu lake.
Kadhalika Haniya amesema HAMAS inakaribisha mkakati wowote wenye irada ya kisiasa na wenye kutekelezeka kivitendo kwa ajili ya kufanikisha usitishaji vita; na pia amesisitiza uthabiti na azma ya harakati hiyo ya muqawama katika kuendeleza mapambano ya kupigania ukombozi wa Palestina.
Siku chache zilizopita, shirika la habari la Anadolu la Uturuki lililinukuu Jarida la Wall Street Journal na kuripoti kuwa, nchi patanishi zimewasilisha pendekezo la kusitisha mapigano kwa miezi 4 kati ya Harakati ya HAMAS na utawala wa Kizayuni, ikiwa ni pamoja na kuachiwa huru mateka wote wa upande wa utawala wa Kizayuni.
Ripoti zinasema kuwa HAMAS inaaminika kuwashikilia karibu mateka 136 wa Israel kufuatia operesheni kubwa iliyotekelezwa na harakati hiyo ya muqawama ya Kimbunga cha Al Aqsa tarehe 7 Oktoba mwaka jana.
HAMAS imekuwa ikisisitiza kuwa kundi hilo la muqawama linataka usitishaji vita katika Ukanda wa Gaza, lakini Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel, Benjamin Netanyahu anataka vita hivyo viendelee na vienee katika eneo kutokana na sababu zake binafsi na za kisiasa.
Utawala huo pandikizi umeshindwa kufikia malengo yake huko Gaza licha ya kuendelea kuwashambuliwa Wapalestina wa eneo hilo lililo chini ya mzingiro kwa mabomu, makombora na kila aina ya silaha tokea Oktoba 7.