UN: Watu wa Gaza wanapambana kila siku ili kuishi
Umoja wa Mataifa umesema kuwa wakazi wa Kipalestina wa Ukanda wa Gaza kila siku wanapambana ili kuweza kuishi.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Msaada kwa Wakimbizi wa Kipalestina, UNRWA limesema katika taarifa yake iliyoituma katiak mtandao wa kijamii wa X kwamba: Kwa kuwa upatikanaji wa maji ya kunywa bado ni changamoto katika Ukanda wa Gaza, watu wengi zaidi wanapoteza maisha kutokana na tatizo la maji na magonjwa ya milipuko katika eneo hilo.
Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaeleza kuwa, wakazi wa ukanda wa Gaza wapatao milioni moja na laki tisa wamelazimika kuwa wakimbizi kufuatia jinai za miezi mitatu za hivi karibuni za utawala wa Kizayuni katika eneo hilo. Asilimia 85 ya wakazi wa Gaza ambao wamekuwa wakimbizi wanakabiliwa na tatizo la dawa za matibabu, maji safi na chakula huku asilimia 60 ya miundomsingi ya ukanda huo ikiwa imeharibiwa kikamilifu.
Katika mazingira hayo, Ujerumani, Uswisi, Italia, Canada, Finland, Australia, Uingereza, Uholanzi, Marekani, Ufaransa, Austria na Japan zimesitisha misaada yake kwa shirika la UNRWA kwa kutegemea madai ya Tel Aviv kwamba baadhi ya wafanyakazi wa shirika hilo wanaunga mkono oparesheni iliyotekelezwa na harakati ya Hamas ya Kimbunga cha Al Aqsa.
Nalo shirika la UNRWA limetangaza katika tathmini yake mpya kuwa imekuwa changamoto kial uchao huko Gaza kupata maji safi na chakula na wakazi wa eneo hilo wanajaribu kila wawezalo ili kuishi.