HAMAS yaiasa ICJ iibebeshe dhima Israel kwa jinai za kivita Gaza
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) imeitaka Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) iuwajibishe utawala wa Kizayuni wa Israel kutokana na jinai za kivita zinazofanywa na utawala huo pandikizi dhidi ya wananchi madhulumu wa Palestina katika Ukanda wa Gaza.
HAMAS imesema katika taarifa kuwa: Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) inapaswa kutoa agizo la wazi na la moja kwa moja la kusimamishwa mauaji ya kimbari na uvamizi wa kikatili unaofanywa na utawala wa Israel dhidi ya watu madhulumu na wasio na ulinzi wa Palestina.
Hapo jana ICJ iliitaka Israel itekeleze haraka na kwa njia inayofaa hatua za muda zilizoainishwa na mahakama katika amri yake ya Januari 26, 2024 ambazo zinahusu eneo lote la Ukanda wa Gaza ikiwa ni pamoja na Rafah.
ICJ ilisema matukio ya hivi karibuni katika Ukanda wa Gaza hasa mji wa kusini wa Rafah yatazidisha kasi ya kile ambacho tayari ni jinamizi la binadamu na matokeo yasiyoelezeka ya kikanda.
Afrika Afrika Kusini imepongeza uamuzi wa jana wa ICJ na kusema kuwa, hatua hiyo ya utawala wa Israel "ni ukiukaji mkubwa na usioweza kurekebishwa wa Mkataba wa Mauaji ya Kimbari na Amri ya Mahakama ya ICJ ya tarehe 26 Januari 2024."
Mnamo Januari 26, ICJ ilitoa uamuzi kuhusu hatua za muda katika kesi ya Afrika Kusini dhidi ya Israel kuhusu mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza. Mahakama hiyo ya Umoja wa Mataifa iliamuru Israel ichukue hatua za haraka kuzuia vitendo vya mauaji ya kimbari na kuhakikisha misaada ya kibinadamu inafika katika eneo hilo.
HAMAS imesema Wapalestina zaidi ya 28,000 wameuawa shahidi tangu ICJ itoe uamuzi wa kutaka kusimamishwa mauaji hayo ya kimbari Gaza, lakini utawala wa Kizayuni umeendelea kupuuza agizo hilo.