Israel yaua Wapalestina zaidi ya 100 waliokuwa wakisubiri misaada Gaza
Wizara ya Afya ya Palestina jana ilitangaza kuwa wanajeshi wa Israel wamewauwa shahidi watu wasiopungua 104 waliokuwa katika umati uliokuwa ukisubiri kupatiwa misaada ya kibinadamu huko kusini mwa Gaza.
Watu walioshuhudia wameeleza kuwa mamia ya Wapalestina walikuwa wakisubiri kugawiwa misaada ya kibinadamu karibu na eneo lq Dowar al Nablusi wakati walipofyatuliwa risasi na wanajeshi wa utawala wa Kizayuni.
Ofisi ya vyombo vya habari ya Palestina imeeleza kuwa utawala wa Kizayuni ulikusudia kutekeleza mauaji hayo ya kutisha dhidi ya Wapalestina. Ofisi hiyo imelithumu jeshi la Israel kwa kuwauwa raia hao wa Kipalestina kwa damu baridi kwa sababu utawala huo ghsibu ulikuwa na taarifa kuhusu uwepo katika eneo hilo wa raia hao wa Kipalestina kwa ajili ya kupatiwa chakula na misaada mingine ya kibinadamu.
Israel iinatekeleza mashambulizi ya kikatili dhidi ya Ukanda wa Gaza tangu Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) itekeleze oparesheni ya kushtukiza dhidi ya maeneo ya utawala wa Kizayuni Oktoba 7 mwaka jana, ambapo Tel Aviv inasema iliuwa raia wake karibu 1,200.
Vita vya utawala wa Kizayuni dhidi ya wakazi wa Ukanda wa Gaza hadi sasa vimewauwa shahidi Wapalestina wasiopungua 30,035 na kujeruhi wengine zaidi ya 70,457.