Mar 24, 2024 06:36 UTC
  • Muqawama wa Iraq: Tumeshambulia kwa droni makao makuu ya wizara ya masuala ya kijeshi ya Israel

Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Iraq imetangaza kuwa imeshambulia makao makuu ya wizara ya masuala ya kijeshi ya utawala wa Kizayuni wa Israel kwa kutumia ndege isiyo na rubani mapema leo Jumapili.

Mwavuli wa makundi ya kupambana na ugaidi nchini Iraq umesema katika taarifa iliyoandikwa kwenye mtandao wake wa Telegram leo Jumapili kwamba: "wapiganaji wa Muqawama wa Kiislamu nchini Iraq alfajiri ya leo Jumapili tarehe 24/03/2024, wameshambulia kwa ndege isiyo na rubani jengo la makao makuu ya wizara ya masuala ya kijeshi ya Israel katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu".
 
Taarifa hiyo ya muqawama wa Kiislamu wa Iraq imeendelea kueleza: "operesheni hii iliyotekelezwa kwa ubora imefanyika katika mikesha hii iliyobarikiwa ili kuthibitisha mwendelezo wetu wa operesheni zetu za kuharibu ngome za adui na ukamilishaji wetu wa awamu ya pili ya oparesheni za kupinga uvamizi  na ukaliaji ardhi kwa mabavu, ambazo zitaongezeka katika mwezi uliobarikiwa wa Ramadhani, kwa kuunga mkono watu wetu huko Ghaza, na ili kukabiliana na mauaji ya halaiki ya Wazayuni dhidi ya raia wasio na ulinzi wa Palestina".
Mhimili wa Makundi ya Muqawama wa Kiislamu

Harakati ya Muqawama wa Kiislamu nchini Iraq imeshafanya oparesheni kadhaa muhimu katika wiki za hivi karibuni, zikiwemo za mashambulizi mengi katika uwanja wa ndege wa Ben Gurion, kituo cha kuzalisha umeme cha Tel Aviv pamoja na bandari kuu za Israel ili kuonyesha mshikamano na watu wa Ghaza.

Siku ya Jumatano, harakati hiyo ilitangaza kuwa wapiganaji wake walishambulia uwanja wa ndege wa Ben Gurion mara mbili ndani ya wiki moja kwa kutumia ndege zisizo na rubani.

Katika mjibizo wa kukabiliana na mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala harmu wa Israel dhidi ya raia wasio na hatia wa Palestina, awamu ya pili ya operesheni za Muqawama imeanza ikijumuisha uwekaji kizuizi cha safari za baharini za Israel katika Bahari ya Mediterania na kulemaza shughuli za bandari za utawala huo haramu.

Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Iraq imetamka bayana kwamba, itaendelea na mashambulizi yake dhidi ya maeneo ya utawala wa Kizayuni wa Israel hadi pale utawala huo utakapokomesha mauaji ya kimbari huko Ghaza.

Muqawama wa Iraq umeshambulia pia kambi kubwa za kijeshi za Marekani nchini Syria na Iraq huku kukiwa na hasira juu ya uungaji mkono wa Washington kwa mashambulizi ya Israel dhidi ya Ghaza.

Zaidi ya Wapalestina 32,000, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, wameshauawa shahidi huko Ghaza hadi sasa, na zaidi ya 74,000 wamejeruhiwa.

Utawala huo dhalimu umeliwekea pia eneo hilo "mzingire kamili" na kuwakatia umeme sambamba na kuwazuilia fueli, chakula na maji Wapalestina wanaoishi katika eneo hilo.../

Tags