Apr 22, 2024 06:19 UTC
  • Kataaib Hizbullah ya Iraq yaanzisha tena mashambulio dhidi ya askari wa Marekani

Vikosi vya Muqawama wa Iraq vimetangaza kuwa, vimeanza tena kutekeleza operesheni za mashambulio dhidi ya vikosi vya majeshi ya Marekani.

Kwa mujibu wa kanali ya habari ya Al Jazeera, Brigedi za Hizbullah ya Iraq (Kataaib Hizbullah) vimetangaza katika taarifa kwamba kuanzishwa tena kwa operesheni za mashambulio dhidi ya Marekani ni matokeo ya kutopigwa hatua yoyote katika mazungumzo kuhusiana na kuondolewa majeshi ya Marekani nchini Iraq yaliyofanyika katika ziara ya Waziri Mkuu wa nchi hiyo Mohammad Shia al- Sudani mjini Washington.
 
Kataaib Hizbullah ni sehemu ya mtandao wa Muqawama wa Kiislamu wa Iraq, ambao mwezi Oktoba mwaka jana ulianzisha mashambulio dhidi ya vikosi vya Marekani vilivyoko Iraq na Syria ukisisitiza kuwa unafanya hivyo kujibu mashambulizi ya kinyama ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina wa Ghaza na kupinga uwepo wa majeshi ya Marekani nchini Iraq na katika eneo.
 
"Kilichofanyika muda mchache nyuma ni mwanzo tu", imeeleza taarifa ya Kataaib Hizbullah ikimaanisha shambulio la roketi la siku ya Jumapili lililolenga kituo cha jeshi la Marekani nchini Syria.
Mohammad Shia al-Sudani

Wiki iliyopita, Mohammad Shia al-Sudani, alikutana na kufanya mazungumzo na Rais Joe Biden wa Marekani katika Ikulu ya White House wakati wa ziara yake nchini humo.

 
Katika mkutano huo, Al-Sudani, akizungumzia suala la kuondoka majeshi ya Marekani nchini Iraq na akasema: "Tutashauriana kuwa na ushirikiano endelevu kwa kuzingatia makubaliano ya mfumo wa kimkakati."
 
Licha ya kufanyika duru kadhaa za mazungumzo ya kimkakati kati ya Baghdad na Washington ili kuhitimisha uwepo wa kijeshi wa Marekani nchini Iraq kutokana na kumalizika vita dhidi ya kundi la kigaidi na ukufurishaji la DAESH (ISIS) na kupitishwa na Bunge la Iraq mpango wa kuwatimua askari wote wa kigeni katika ardhi ya nchi hiyo, Marekani imeukiuka mpango huo wa bunge na kuendelea kubaki nchini Iraq.
 
Hivi sasa, wanajeshi wa Kimarekani wako katika vituo viwili vya kijeshi nchini Iraq, muhimu zaidi kati ya hivyo kikiwa ni cha Ain al-Asad kilichoko mkoani Al- Anbar.../

 

Tags