Mfumo wa huduma ya afya wa Gaza unakaribia kusambaratika kabisa
Wizara ya Afya ya Palestina katika Ukanda wa Gaza, ambayo inaendelea kustahamili vita vya mauaji ya kimbari vinavyotekelezwa na utawala haramu wa Israel katika eneo hilo imeonya kuhusu kusambaratika kabisa mfumo mzima wa afya katika eneo hilo.
Katika taarifa leo Jumatatu, wizara hiyo imesema: "Tumebakisha saa chache tu kabla ya kusambaratika kabisa mfumo wa afya katika Ukanda wa Gaza."
Wizara hiyo imehusisha uwezekano huo nchungu na “kushindwa kufikishwa mafuta yanayohitajika kuendeshea jenereta za umeme katika hospitali na magari ya kubebea wagonjwa, na kuwasafirisha wafanyakazi.”
Mnamo Mei 7, jeshi katili la Israel lilichukua udhibiti kamili wa kivuko cha Rafah kusini mwa Gaza, eneo ambalo linapakana na Misri na hutumika kama sehemu kuu ya kuingiza misaada pamoja na mafuta Gaza.
Hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za utawala huo ghasibu za kuudhibiti mji wa Rafah, kwa madai kuwa eti ni ngome kuu ya "mwisho" ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas.
Zaidi ya Wapalestina 35,000, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, wamekufa kutokana na mashambulizi ya kikatili ya kijeshi ya Israel dhidi ya Gaza yaliyoanza Oktoba 7.
Vita hivyo tayari vimeathiri vibaya mfumo wa afya wa Gaza kwa kuwaua takriban wafanyikazi 500 wa sekta ya afya na kusababisha uharibifu wa hospitali nyingi katika hilo hilo.