Familia za wanajeshi waliouawa zamshambulia Waziri wa Usalama wa Israel
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i111730-familia_za_wanajeshi_waliouawa_zamshambulia_waziri_wa_usalama_wa_israel
Familia za wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel waliouawa vitani Ukanda wa Gaza zimemshambulia Itamar Ben- Gvir Waziri wa Usalama wa Ndani wa utawala wa Kizayuni.
(last modified 2024-05-13T23:38:03+00:00 )
May 13, 2024 23:38 UTC
  • Familia za wanajeshi waliouawa zamshambulia Waziri wa Usalama wa Israel

Familia za wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel waliouawa vitani Ukanda wa Gaza zimemshambulia Itamar Ben- Gvir Waziri wa Usalama wa Ndani wa utawala wa Kizayuni.

Shirika la habari la Palestina la Sama'a limeripoti kuwa, familia za wanajeshi wa utawala wa Kizayuni waliouawa katika vita vya Ukanda wa Gaza zimemshambulia Itamar Ben -Gvir Waziri wa Usalama wa Ndani wa Israel katika eneo la makaburi ya wanajeshi katika eneo la Ashdod huku wakipiga nara "mtenda jinai, 'mtenda jinai'.  

Ben Gvir ni kati ya mawaziri wenye misimamo mikali wa serikali ya Israel wanaochochea vita na mauaji ya kimbari dhidi ya watu wa Gaza licha ya matakwa ya ndani ya nje ya kusimamisha vita. 

Itamar Ben Gvir 

Waziri huyo wa Usalama wa Ndani wa Israel ametishia kuwa atatayarisha mazingira ya kusambaratika serikali ya mseto ya utawala wa Kizayuni ikiwa vita vya Gaza vitasitishwa.    

Uungaji mkono kwa Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni, Benjamini Netanyahu katika duru za kisiasa umepungua pakubwa huku weledi wa masuala ya kisiasa wakiutathmini mustakbali wake wa kisiasa kuwa wenye kuyumba baada ya kufeli mkabala wa oparesheni ya wanamuqawama wa Palestina ya Kimbunga cha al Aqsa na kushindwa kuwakomboa mateka wake.