Yemen yaonya inaweza kulenga shabaha za adui 'ambazo hawezi hata kuzifikiria'
Jeshi la Yemen limeonya kuwa huenda likazidisha mashambulizi yake ya kuiunga mkono Palestina iwapo utawala wa Israel utaendelea na vita vyake vya mauaji ya halaiki katika Ukanda wa Gaza.
Msemaji wa jeshi hilo Brigedia Jenerali Yahya Saree alitoa onyo hilo jana Jumatatu.
Amesisitiza kwa kusema: "Gaza ni mstari mwekundu kwetu, mstari mwekundu. malengo, maeneo matakatifu, na Uislamu wetu ni mistari myekundu kwetu, na wala hatutahadiliana na yeyote kuhusu masuala haya.”
Saree ameendelea kusema: "Tunalenga mambo ambayo adui hajayafikiria na wala hawezi kuyafikiria, mambo ambayo watu wa Yemeni na wa mataifa ya Kiarabu na Kiislamu hawawezi kuyafikiria."
Yemen ilianzisha mashambulizi hayo baada ya Oktoba 7, wakati utawala wa Israel ulipoanzisha vita dhidi ya Gaza, ambapo hadi sasa vimeua zaidi ya Wapalestina 35,000 wengi wao wakiwa wanawake na watoto.
Jeshi la Yemen lilianzisha operesheni ya kuzilenga meli za Israel au zile zinazoelekea kwenye bandari za ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu (Israel), ambazo zinapitia katika maji ya Yemen.
Hatua kwa hatua lilipanua operesheni hiyo kwa kulenga maeneo ndani ya ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na meli zinazopitia Bahari ya Hindi huku utawala wa Israel ukikataa matakwa yake ya kusimamisha vita na mzingiro dhidi ya Gaza.
Mapema mwezi Mei, Saree alitangaza kuanza awamu ya nne ya operesheni ya kuunga mkono Palestina, akisema jeshi la Yemen litalenga meli zote zinazoelekea bandari za Israel "katika Bahari ya Mediterania."
Vile vile ameonya kuwa jeshi la Yemen litaziwekea vikwazo meli zote za makampuni yanayohusika na kubeba mizigo na kuingia katika bandari za Israel, bila kujali utaifa wazo.