Wapalestina: Tuko tayari kwa 'vita vya muda mrefu' Rafah
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i111908-wapalestina_tuko_tayari_kwa_'vita_vya_muda_mrefu'_rafah
Tawi la kijeshi la Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) limetangaza kuwa Wapalestina wako tayari kwa vita vya muda mrefu, na kuahidi kukabiliana na uvamizi wa nchi kavu wa Israel dhidi ya Rafah, kusini mwa Ukanda wa Gaza na kwingineko.
(last modified 2024-05-18T09:13:25+00:00 )
May 18, 2024 09:13 UTC
  •  Abu Obeida
    Abu Obeida

Tawi la kijeshi la Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) limetangaza kuwa Wapalestina wako tayari kwa vita vya muda mrefu, na kuahidi kukabiliana na uvamizi wa nchi kavu wa Israel dhidi ya Rafah, kusini mwa Ukanda wa Gaza na kwingineko.

"Licha ya nia yetu kamili ya kukomesha uchokozi dhidi ya watu wetu, tumejitayarisha kwa vita vya muda mrefu dhidi ya adui, tukiwaburuta kwenye kinamasi ambapo hawatapata chochote isipokuwa vifo vya askari wao na kukamatwa mateka maafisa wa jeshi lao", amesema msemaji wa Qassam Brigades, Abu Obeida, katika ujumbe wa video.

Abu Obeida amesisitiza kuwa: "Hii ni kwa sababu sisi ni watu wa ardhi hii na ni wamiliki wake halali."

Qassam Brigades

Matamshi yake yanakuja huku mapigano yakipamba moto huko Gaza, na jeshi la Israel likizidisha mashambulizi ya nchi kavu katika mjini Rafah licha ya wasiwasi wa kimataifa wa kuuawa mamia ya maelfu ya Wapalestina waliokimbia makazi yao na kupewa hifadhi katika mji huo wa kusini mwa Ukanda wa Gaza.

Abu Obeida amesema, katika siku 10 zilizopita, wapiganaji wa Kipalestina wameharibu magari 100 ya kijeshi ya Israel, ikiwa ni pamoja na vifaru na tingatinga.

Vilevile wapiganaji wa Kipalestina wameua idadi kubwa ya wanajeshi wa Israel japokuwa utawala huo ghasibu unaficha takwimu halisi za idadi ya askari wake wanaouawa huko Gaza. 

Msemaji wa Qassam Brigades amesema, jeshi la Israel limefanya makosa makubwa kwa kuamua kuanzisha uvamizi wa nchi kavu katika maeneo ya Rafah, kitongoji cha Zaitoun na kambi ya wakimbizi ya Jabalia, na kwamba suala hilo linawafanya wanajeshi wa Israel kuwa shabaha rahisi kwa wapigania ukombozi wa Palestina.