Sheikh Naeem Qassim: Hizbullah haijaghafilika katu na Israel
Naibu Katibu Mkuu wa harakati ya muqawa wa Kiislamu ya Lebanon Hizbullah, amesema muqawama katu haujaghafilika na njama na vitisho vya utawala wa Kizayuni wa Israel.
Sheikh Naeem Qassim amesema tangu Hizbullah ilipoanza kushiriki kijeshi nchini Syria, muda wote imekuwa ikifuatilia nyendo na harakati za utawala wa Kizayuni.
Mbali na kutangaza utayari wa Hizbullah kukabiliana na shambulio lolote linaloweza kufanywa na jeshi la Israel dhidi ya Lebanon, Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah amesema:"Katika kipindi hiki Israel haina uthabiti, na inategemea matukio ya nje kwa ajili ya kuimarisha nguvu zake".
Kuhusiana na uingiliaji kijeshi wa Saudia nchini Syria, Sheikh Naeem Qassim amesema:"Kwamba Saudia imetangaza kuwa itajiingiza kijeshi Syria kupitia kile kinachoitwa muungano wa kimataifa unaoongozwa na Marekani, hii maana yake ni kwamba kuna mpango ulioandaliwa na Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati ambao Saudia inataka kuwa mwakilishi wa utekelezaji wake".../