Kushambulia Rafah; kipaumbele cha Israeli na kupuuzwa matakwa ya kimataifa
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i112378-kushambulia_rafah_kipaumbele_cha_israeli_na_kupuuzwa_matakwa_ya_kimataifa
Huku ukiwa umepuuza matakwa na maonyo ya kimataifa kuhusu athari na matokeo hatari ya kibinadamu ya kushambuliwa mji wa mpakani wa Rafah ulioko kusini mwa Ukanda wa Gaza, utawala wa Kizayuni umetuma vikosi vya kivita katika eneo hilo, ambapo vinaua kikatili wakazi wake bila kujali lolote.
(last modified 2024-05-30T23:07:16+00:00 )
May 30, 2024 23:07 UTC
  • Kushambulia Rafah; kipaumbele cha Israeli na kupuuzwa matakwa ya kimataifa

Huku ukiwa umepuuza matakwa na maonyo ya kimataifa kuhusu athari na matokeo hatari ya kibinadamu ya kushambuliwa mji wa mpakani wa Rafah ulioko kusini mwa Ukanda wa Gaza, utawala wa Kizayuni umetuma vikosi vya kivita katika eneo hilo, ambapo vinaua kikatili wakazi wake bila kujali lolote.

Mji wa Rafah unaopakana na Misri una kivuko cha pekee ambacho kimekuwa kikitumiwa na Wapalestina wanaoishi katika Ukanda wa Gaza kama njia pekee ya kuwasiliana na  ulimwengu wa nje. Baada ya kuanza duru mpya ya mashambulizi ya jeshi ya Israel huko Gaza (Oktoba 7) kwa kisingizio cha kupambana na makundi ya muqawama ya Palestina, sasa eneo hilo limekuwa makazi muhimu ya karibu nusu ya watu milioni 1.2 wa Ukanda wa Gaza, ambao wamekimbilia eneo hilo finyu kutoka maeneo mengine yaliyoshambuliwa na Wazayuni. Hiyo ndio maana nchi, taasisi na mashirika ya kimataifa yakatahadharisha kuhusu matokeo hatari ya kushambuliwa Rafah na kusema kuwa, iwapo operesheni za kijeshi za Wazayuni zitatekelezwa katika eneo hilo, mji huo utashuhudia mauaji ya kimbari ya Wapalestina ambayo hayajawahi kushuhudiwa tena huko nyuma.

Mashambulizi ya Israel kwenye mji wa mpakani wa Rafah kusini mwa Gaza

Kuna ripoti za kuwasili kwa wingi vikosi vya jeshi la Israel huko Rafah, huku Wapalestina wasiopungua 45, ambao wengi wamekuwa wanawake na watoto, wakiuawa shahidi na wengine 250 wakiijeruhiwa katika shambulio la jinai la Wazayuni kwenye kambi ya wakimbizi katika eneo hilo siku ya Jumapili usiku. Ingawa shambulio hilo limekemewa na kulaaniwa na nchi nyingi za dunia na hata waungaji mkono wa jadi wa Ulaya wa utawala huo, lakini sisitizo la utawala wa Tel Aviv la kupanua wigo wa vita hadi Rafah linaonyesha utambulisho wa jinai na unyama wa utawala huo wa kibaguzi katika kuendeleza mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina.

Onyo la ulimwengu kuhusu matokeo hatari ya shambulio kubwa la Israel dhidi ya Rafah

Wazayuni wanafuatilia mpango wa kushambulia na kuharibi kabisa mji wa Rafah katika hali ambayo Mahakama ya Kimataifa ya Haki Ijumaa iliyopata iliamuru kusitishwa mara moja operesheni za Israel katika eneo hilo na kutaka kufunguliwa tena kivuko cha Rafah ili kuwezesha misaada ya kibinadamu kuingia Gaza. Sisitizo la Wazayuni la kutaka kupanua wigo wa vita na jinai katika mji wa Rafah linatekelezwa, huku mashambulizi ya kikatili ya utawala huo ambayo yamekuwa yakiendelea katika maeneo mengine ya Gaza kwa miezi 8 iliyopita yakiwa hayajafanikisha lolote zaidi ya kusababisha mauaji ya kimbari, uharibifu wa miundomsingi, ukiukaji wa sheria za kimataifa, ulipuaji wa mashirika ya misaada na kuwaweka njaa watu wa eneo hilo. Kwa mujibu wa takwimu za karibuni Wapalestina zaidi ya 36,000 wameuawa shahidi na wengine 81,000 wamejeruhiwa tangu kuanza mauaji ya umati ya utawala wa Kizayun dhidi ya Wapalestina tarehe 7 Oktoba, wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto. Uharibifu wa asilimia 80 ya nyumba na miundombinu ya Gaza ni mafanikio mengine kwa Wazayuni katika kipindi hiki.

Uharibifu mkubwa wa miundombinu ya Ukanda wa Gaza katika mashambulizi ya Israel

Mauaji haya ya kimbari ambayo hayajawahi kutokea tena yamepingwa na kulaaniwa mara kwa mara na mashirika na shakhsia wa kimataifa, hasa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. Francesca Albans, Ripota Maalum wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Masuala ya Palestina, hivi karibuni alielezea masikitiko yake kwa kutojali utawala wa Kizayuni kuhusiana na matokeo ya jinai unazozifanya huko Gaza na kusisitiza kuwa utawala huo unafanya jinai hizo na kukiuka wazi wazi sheria za kimataifa kwa uungaji mkono wa baadhi ya madola makubwa duniani na hasa Marekani. Kwa hakika, mbali na kushambulia kwa mabomu na makombora maeneo tofauti ya Gaza, utawala wa Kizayuni pia unatumia njaa na kuzuia kufikishwa chakula na dawa katika eneo hilo kama silaya ya kushadidisha mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina huko Gaza. Hii ni katika hali ambayo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa katika azimio lake la karibuni limeutaka utawala huo wa Kizayuni kuchukua hatua za lazima ili kuhakikisha kuwa misaada ya kimsingi inawafikia Wapalestina katika ukanda huo. Wakati huo huo utawala wa Kizayuni ukiungwa mkono na Marekani unaendelea kushambulia eneo hilo huku ukivuruga ufikishaji wa misaada ya kimataifa ya kibinadamu huko Gaza. Kuunga mkono jinai za Wazayuni na kupuuza ukandamizaji unaofanywa na utawala huo dhidi ya Wapalestina kunathibitisha wazi misimamo ya undumakuwili ya Wamagharibi kuhusu kadhia ya Palestina na unafiki wao kuhusiana na suala zima la haki za binadamu.