Adhabu kwa wanachuo wa Marekani wanaounga mkono Palestina
Makumi ya wanachuo wa Chuo Kikuu cha Chicago nchini Marekani wameondoka katika chuo hicho wakipinga hatua ya bodi ya wakurugenzi ya kukataa kutoa shahada za wanafunzi wanaounga mkono Palestina.
Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA- baada ya Chuo Kikuu cha Marekani cha Chicago kukataa kutoa shahada kwa wanafunzi wake wanne kutokana na kushiriki katika maandamano dhidi ya utawala haramu wa Israel makumi ya wanafunzi waliandamana wakiwa na bendera za Palestina mikononi mwao na wengine wakiwa na vitambaa vya Palestina walionyesha mshikamano na Wapalestina huku wakiimba: Kkomesheni Mauaji ya Kimbari.
Kulingana na Muungano wa Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Chicago, wanafunzi wanne waliarifiwa kwa barua pepe katika siku za hivi karibuni kwamba vyeti vyao havitatolewa mpaka uamuzi wa matokeo ya mchakato wa kinidhamu unaohusiana na malalamiko yanayotokana na uwekaji wa mahema ya maandamano kwenye chuo kikuu utakapotangazwa.
Maandamano ya wanafunzi hao wanaounga mkono Palestina na kulaani jinai za utawala katili wa Kizayuni yaliyoanza katika Chuo Kikuu cha Columbia huko Marekani licha ya kukabiliwa na ukandamizaji na ukatili wa mamlaka ya Marekani yalienea kwa mara ya kwanza katika vyuo vikuu vingine vya nchi hiyo kikiwemo cha Yale, Harvard, Texas, na Southern California. Aidha wimbi la maandamano hayo lilifika katika vyuo vikuu vya nchi zingine za magharibi ikiwa ni pamoja na Ufaransa, Ujerumani, Kanada, Uingereza na Australia.
Utawala wa Kizayuni kwa ungwaji mkono na Marekani na mbele ya macho ya mashirika ya kimataifa na ya kutetea haki za binadamu umekuwa ukifanya mauaji ya kimbari dhidi ya watu wasio na ulinzi wa eneo hilo kwa kuushambulia Ukanda wa Gaza kwa takriban miezi minane sasa.
Wizara ya Afya ya Palestina ilitangaza katika Ukanda wa Gaza kwamba tangu kuanza kwa mashambulizi hayo ya kinyama ya utawala katili wa Kizayuni tangu tarehe 7 Oktoba, 2023 mwaka jana watu zaidi ya 36,379 wameuawa shahidi na wengine 82,407 wamejeruhiwa.