Mamia ya Walebanon wameuawa shahidi katika mashambulio ya utawala wa Kizayuni
Jun 06, 2024 03:20 UTC
Wizara ya Afya ya Lebanon imetangaza kuwa watu 400 wameuawa shahidi tangu jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel lilipoanzisha mashambulizi dhidi ya nchi hiyo mwezi Oktoba, 2023.
Kwa mujibu wa IRNA, Wizara ya Afya ya Lebanon imesema, tangu yalipoanza mashambulizi ya jeshi la utawala wa Kizayuni nchini humo Oktoba mwaka jana watu 400 wameuawa shahidi na wengine 1,603 wamejeruhiwa.
Wizara ya Afya ya Lebanon imebainisha kuwa tokea wakati huo hadi sasa watu elfu 94 wamelazimika kuyahama makazi yao.
Wakati huo huo, shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limetangaza katika ripoti yake liliyotoa jana Jumatano kwamba tangu Oktoba 7, 2023 hadi sasa, jeshi la Israel limetumia silaha zenye fosforasi nyeupe dhidi ya vitongoji visivyopungua 17 kusini mwa Lebanon, na kuhatarisha maisha ya raia, mbali na wengi waliolazimika kuyahama makazi yao.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, fosforasi nyeupe ni mada ya kemikali ambayo hutumiwa katika risasi za mizinga, mabomu na makombora, na endapo itapata hewa ya oksijeni huwaka; na madhara yake husababisha kifo kutokana na kuunguza sana na kuyeyusha viungo vya mwili na kuacha majeraha makubwa ambayo makovu yake hubaki kwenye ngozi ya mtu milele.
Ripoti hiyo imebainisha kuwa, kutumiwa kwa kiwango kikubwa na Israel fosforasi nyeupe kusini mwa Lebanon kunatilia nguvu ulazima wa kuwepo sheria kali za kimataifa za kuzuia utumiaji wa silaha zinazotoa moto.
Kufuatia uungaji mkono ulioonyeshwa na harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon kwa makundi ya Muqawama ya Palestina katika kukabiliana na jinai za kutisha za utawala wa Kizayuni huko Ukanda wa Ghaza, kwa miezi kadhaa sasa jeshi la utawala huo linayalenga maeneo ya makazi ya watu kusini mwa Lebanon kwa mashambulizi ya anga na mizinga.../
Tags