Jun 10, 2024 03:22 UTC
  • Malaysia yaziasa nchi za D-8 zikate uhusiano wa kiuchumi na Israel

Waziri wa Mambo ya Nje wa Malaysia amezitaka nchi wanachama wa kundi la D-8 kuvunja uhusiano wao wa kiuchumi na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Mohamad Hasan, Waziri wa Mambo ya Nje wa Malaysia alitoa mwito huo jana Jumapili katika mkutano maalumu wa mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama wa kundi hilo la nchi zinazostawi kiuchumi la D-8 mjini Istanbul, Uturuki.

Ameziasa nchi wanachama wa jumuiya hiyo ya ushirikiano wa kiuchumi kutoipa Israel msaada wa aina yoyote akisisitiza kuwa, hatua hiyo huenda ikaufadhili kijeshi utawala wa Kizayuni na kuushajiisha uendelee kukalia kwa mabavu ardhi za Wapalestina.

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi za juu wa Malaysia amebainisha kuwa, kuna haja ya kubuni na kufanya rasmi ushirikiano baina ya kundi la D-8 na taifa la Palestina. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Uturuki, Pakistan, Malaysia, Indonesia, Bangladesh, Misri na Nigeria ni nchi 8 wanachama wa awali wa kundi hilo ambalo limebadilika na kuwa jumuiya. 

Waziri wa Mambo ya Nje wa Malaysia amesema nchi yake pamoja na nchi nyingine wanachama wa D-8 zimetangaza bayana kuunga mkono kadhia ya Palestina, katika taarifa ya pamoja iliyotolewa katika mkutano maalumu wa mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama wa D-8 mjini Istanbul.

Wananchi wa Malaysia wakichoma moto bendera za Israel

Viongozi wa Malaysia wamekuwa wakitangaza bayana kuunga mkono kwa dhati muqawama wa makundi ya Wapalestina dhidi ya mashambulizi ya kinyama ya utawala wa Kizayuni wa Israel.

Hivi karibuni, Anwar Ibrahim, Waziri Mkuu wa Malaysia wakati akitetea uhusiano wa nchi yake na Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS, alisisitiza kuwa, operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa ulikuwa ni mwanzo wa hatua ya kukabiliana na miongo kadhaa ya "ukatili, uporaji na unyang'anyi wa milki" uliofanywa na Israel dhidi ya Wapalestina.

 

Tags