Jun 30, 2024 06:13 UTC
  • UN  yakosoa ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan

Mratibu Maalumu wa Umoja wa Mataifa katika Masuala ya Amani ya Asia Magharibi, akielezea wasiwasi wake juu ya kuendelea ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, ameutaja upanuzi wa ujenzi wa vitongoji vya walowezi katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu kuwa ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa.

Bezalel Smotrich, Waziri wa Fedha wa utawala wa Kizayuni hivi karibuni, katika kukabiliana na ongezeko la kukubalika kwa zaidi ya nchi 140 kutokana na kutambuliwa taifa la Palestina, alipendekeza kuwawekea vikwazo maafisa wa mamlaka ya ndani ya Palestina pamoja na kuhalalisha kujengwa kwa  vitongoji vitano vya walowezi katika eneo hilo la Ukingo wa Magharibi wa mto Jordan.

Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, Tor Vansland, mratibu maalum wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya amani katika eneo la Magharibi mwa Asia, aliandika katika mtandao wa kijamii wa X kwamba; tangazo la hivi karibuni la mmoja wa mawaziri wa baraza la usalama la utawala wa Israel kuhusu kuhalalisha upanuzi wa vitongoji vya walowezi katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, kwa mujibu wa sheria za Israel unatia wasiwasi sana.

Vile vile amesisitiza kwamba; hatua hizo zinazoidhoofisha Mamlaka ya ndani ya Palestina na kuimarisha upanuzi wa vitongoji vya walowezi katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan ambao umesababisha kushadidi kwa mivutano na kudhoofisha uwezekano wa kupatikana amani kwa msingi wa pande mbili na suluhisho la serikali mbili.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, vikwazo vya Israel dhidi ya Mamlaka ya ndani ya Palestina vinafuatia mashtaka dhidi ya utawala wa Kizayuni katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) na uwezekano wa kutolewa hati ya kukamatwa Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu na Waziri wa Vita Yoav Gallant.

Tags