Askari kadhaa wa Israel waangamizwa katika mashambulizi ya Hizbullah
(last modified 2024-09-19T14:09:33+00:00 )
Sep 19, 2024 14:09 UTC
  • Askari kadhaa wa Israel waangamizwa katika mashambulizi ya Hizbullah

Wanajeshi kadhaa wa utawala wa Kizayuni wa Israel wameangamizwa huku wengine wengi wakijeruhiwa katika mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Harakati ya Muqawama ya Hizbullah ya Lebanon.

Duru za habari zinaarifu kuwa, katika shambulio la Hizbullah lililolenga eneo la kijeshi la al-Marj karibu na mpaka wa Lebanon, wanajeshi wasiopungua 2 wa Israel waliuawa na wengine zaidi ya 15 kujeruhiwa.

Aidha katika mfululizo wa mashambulizi ya Hizbullah kaskazini mwa ardhi za Wapalestina zinazokaliwa kwa mabavu (Israel) mwanajeshi mmoja wa Israel aliuawa na wengine zaidi ya 8 kujeruhiwa.

Wakati huo huo, droni za Hizbullah leo Alkhamisi zimelenga kambi ya kijeshi ya Israeli huko Beit Hillel karibu na Kiryat Shmona. Askari kadhaa wa Kizayuni wamejeruhiwa katika shambulio hilo.

Kadhalika eneo la Yaara lililoko Magharibi mwa Galilaya, pia limeshambuliwa na ndege zisizo na rubani za Hizbullah na kuisababishia hasara kubwa Israel.

Harakati ya Hizbullah ya Lebanon imeapa kuendeleza mashambulizi yake dhidi ya utawala haramu wa Israel kwa ajili ya kuwatetea watu wa Ukanda wa Gaza, ambao wanaendelea kuuawa kikaktili katika mauaji ya kimbari ya Israel, ikisisitiza kwamba ukatili wa hivi karibuni wa utawala huo ulioua watu kadhaa nchini Lebanon utaimarisha azma yake ya kuendeleza njia ya mapambano na muqawama.

Hizbullah imekuwa ikifanya mashambulizi karibu ya kila siku dhidi ya Israel ikiwa ni kuunga mkono na kuwatetea watu wa Ukanda wa Gaza na mashambulizi makali ya Israel ambayo yamekuwa yakilenga ardhi ya Lebanon tangu kuanzishwa kwa vita mauaji ya kimbari katika ardhi ya Palestina.

Tags