Israel yaua watu wengine 72 na kujeruhi 400 Lebanon, Hizbullah yajibu mapigo kwa makombora
(last modified 2024-09-26T06:47:23+00:00 )
Sep 26, 2024 06:47 UTC

Utawala wa Kizayuni wa Israel umewaua shahidi watu wasiopungua 72 na kuwajeruhi wengine 400 nchini Lebanon katika siku ya tatu mtawalia ya mashambulizi ya kiwendawazimu unayofanya katika ardhi ya nchi hiyo sambamba na makabiliano yanayoendelea baina yake na harakati ya Muqawama ya Hizbullah.

Wizara ya Afya ya Lebanon imetoa takwimu za idadi hiyo ya watu waliouawa shahidi na kujeruhiwa, ikisema maafa hayo yametokana na mashambulizi ya anga yaliyofanywa na jeshi la utawala wa Kizayuni dhidi ya nchi hiyo mapema jana.
 
Mashambulizi hayo ya anga yamejumuisha mashambulizi ya nadra kufanywa dhidi ya vijiji vya Joun na Maaysra, ambayo ni maeneo ya milimani nje ya ngome za jadi za harakati ya Hizbullah kusini na mashariki mwa Lebanon.
 
Wizara ya Afya ya Lebanon imebainisha katika taarifa yake kwamba shambulio dhidi ya kijiji cha Joun kilichoko katika milima ya Chouf kusini mashariki mwa Beirut lilisababisha vifo vya watu wanne, na shambulio jengine dhidi ya Maaysra, kijiji chenye wakazi wengi Waislamu wa madhehebu ya Shia, kilichoko yapata kilomita 25 kaskazini mwa Beirut, limeua shahidi watu watatu.
 
Watu wengine tisa waliuawa shahhidi katika shambulio dhidi ya kusini mwa Lebanon, na wengine saba upande wa mashariki.
 
Wakati huo huo, Umoja wa Mataifa umeripoti kuwa watu wapatao 90,000 wamelazimika kuyahama makazi yao nchini Lebanon kutokana na mashambulizi yanayoendelea kufanywa na jeshi la utawala wa Kizayuni.
Wanamuqawama wa Hizbullah

Katika upande mwingine, Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Lebanon, Hizbullah imetangaza kuwa imerusha kombora la balestiki lililofika Tel Aviv kwa mara ya kwanza.

Hizbullah imeeleza pia kuwa, imefanya mashambulio ya makombora yaliyolenga Sa'ar kibbutz karibu na Nahariya kaskazini mwa Israel, na kujeruhi watu kadhaa, kulingana na ripoti za vyombo vya habari vya ndani.

Tangu harakati ya Muqawama ya Palestina Hamas ilipofanya Operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa mnamo Oktoba 7, 2023, Hizbullah na Israel zimekuwa zikikabiliana kwa mashambulio ya mpakani.

Mnamo Septemba 23, jeshi la utawala wa Kizayuni lilifanya shambulio la kinyama kusini na mashariki mwa Lebanon, na kuwaua shahidi zaidi ya watu 550, ikiwa ni idadi kubwa zaidi ya watu kuuawa katika siku moja tangu vita vya mwaka 2006.../

 

Tags