Oct 01, 2024 03:19 UTC
  • HAMAS: Tumeangamiza idadi kubwa ya askari wa Israel Gaza

Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS imetangaza habari ya kuangamiza idadi kubwa ya wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel kusini mwa Ukanda wa Gaza.

Tovuti ya habari ya al-Jazeera imenukuu taarifa ya Brigedi za Izzuddin Qassam, tawi la kijeshi la Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS inayosema kuwa, wanajeshi wengi wa Kizayuni wameuawa na kujeruhiwa baada ya kuripukiwa na mabomu yaliyotengwa ardhini na wanamuqawama wa Qassam katika eneo la al-Fakhari, mashariki mwa Khan Younis, kusini mwa Gaza.

Makumi ya operesheni za kijeshi zimetekelezwa dhidi ya jeshi vamizi la Kizayuni katika maeneo mengi ya Gaza.

Haya yanajiri huku askari wa jeshi la utawala wa Kizayuni wakianzisha operesheni ya nchi kavu nchini Lebanon.

Wizara ya Afya ya Lebanon imesema kuwa, watu wasiopungua 95 waliuawa jana Jumatatu pekee katika operesheni ya wanajeshi wa Kizayuni, katika viunga vya kusini mwa Beirut.  

Israel tokea Septemba 23 imeendelea kushambulia kwa mabomu makazi ya raia katika mji mkuu wa Lebanon, Beirut na kuua shahidi idadi kubwa ya watu akiwemo Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah, Sayyid Hassan Nasrullah.

Tags