HAMAS: Ghaza haitasalimu amri; Muqawama ndio utakaotoa masharti
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i128152
Kiongozi mwandamizi wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS Izzat al-Rishq amesema, Ghaza haitasalimu amri, na ni Muqawama ndio utakaotoa masharti, si utawala wa Kizayuni wa Israel.
(last modified 2025-07-10T07:37:37+00:00 )
Jul 10, 2025 07:35 UTC
  • HAMAS: Ghaza haitasalimu amri; Muqawama ndio utakaotoa masharti

Kiongozi mwandamizi wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS Izzat al-Rishq amesema, Ghaza haitasalimu amri, na ni Muqawama ndio utakaotoa masharti, si utawala wa Kizayuni wa Israel.

Katika taarifa aliyoweka kwenye akaunti yake ya Telegram, al-Rishq ameyaelezea matamshi ya hivi karibuni ya waziri mkuu wa utawala wa kizayuni Benjamin Netanyahu - kuhusu kuachiliwa mateka wote na kujisalimisha Hamas – kuwa ni onyesho linaloakisi "kushindwa kisaikolojia na kujidanganya, na si uhalisia katika medani ya vita."

Al-Rishq ameongezea kwa kusema: "baada ya viongozi wa adui kukiri kushindwa kikamilifu kuwapata mateka wao kupitia operesheni za kijeshi, imedhihirika kuwa njia pekee ya kupata kuachiliwa kwao ni kupitia mapatano mazito na Muqawama."

Kiongozi huyo mwandamizi wa Hamas amesisitiza kuwa, Muqawama wa Palestina tayari umeshaonyesha muelekeo na masharti mapya yanayotokana na hali halisi kwenye medani ya vita na utaendelea kufanya hivyo.

Hayo yanajiri huku jeshi la utawala wa Kizayuni likiendeleza vita vya kinyama na mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Ghaza. Ripoti za hivi punde za eneo hilo la Palestina inayokaliwa kwa mabavu lililowekewa mzingiro zinaeleza kuwa, tokea alfajiri ya leo hadi sasa, jeshi la utawala haramu wa Israel limeshawaua shahidi Wapalestina wengine wasiopungua 24 katika maeneo mbalimbali ya Ghaza.

Wizara ya Afya ya Palestina katika Ukanda wa Ghaza imetangaza kuwa, Wapalestina wasiopungua 57,575 wameshauwa shahidi na wengine 136,879 wamejeruhiwa tangu utawala wa Kizayuni ulipoanzisha vita dhidi ya Ghaza Oktoba, 2023.../