Syria yatoa tena onyo kali kwa Saudia
Spika wa Bunge la Syria ametoa onyo kali kwa ukoo wa Aal Saud unaojigamba kuwa utatuma wanajeshi wake nchini Syria.
Muhammad Jihad al Laham ametoa onyo hilo leo wakati alipohojiwa na gazeti la nchini Lebanon la Sada al Balad na kusema kuwa, kama Saudi Arabia itathubutu kutuma wanajeshi wake nchini Syria, basi ikubali pia maafa itakayopata, kwani wanajeshi hao watahesabiwa ni wanajeshi vamizi, na watarudi kwao wakiwa kwenye majeneza.
Jihad al Laham amegusia pia kuzimwa njama zote za maadui wa Syria na kusema kuwa, inachotaka serikali ya Syria ni kufanyika uchaguzi kwa wakati unaofaa ili wananchi wenyewe waamue, lakini wapinzani wa serikali na wale waliojipachika jina la wanamapinduzi, wanakwamisha kwa kila njia jitihada hizo za serikali ya Damascus.
Amesema, Rais Bashar al Assad amechaguliwa kihalali na wananchi na kwamba njama zozote zinazoendeshwa na Qatar, Uturuki, Saudia na waungaji mkono wao za kujaribu kuiangusha serikali ya Syria iliyochaguliwa na wananchi, zitashindwa tu.
Itakumbukwa kuwa, tangu mwanzoni mwa mwezi huu wa Februari, Suadia imekuwa ikidai kuwa itatuma wanajeshi wake nchini Syria hata kama serikali ya Syria haitatoa idhini.