Wanazuoni Bahrain wakosoa ukandamizaji dhidi ya Mashia wanaomboleza
Wanazuoni wakuu wa Kiislamu nchini Bahrain wamelaani ukandamizaji na dhulma zinazofanywa na watawala wa Aal-Khalifa dhidi ya Waislamu wa madhehenu ya Shia hususan wakati huu wanapofanya marasimu mbali mbali ya kukumbuka kuuawa shahidi Imam Hussein AS, mjukuu wa Mtume Mtukufu SAW.
Taarifa ya maulamaa wa Bahrain imesema kuwa, hatua ya maafisa usalama wa Bahrain ya kuyavamia na kuyahujumu maeneo yanapofanyika marasimu hayo ya kidini ni kitendo kiovu, cha woga na kisichokubalika.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa, kuvunja mabango na bendera zinazohusiana na maadhimisho ya kumbukumbu ya kuuawa shahidi mjukuu wa Mtume SAW kunakiuka misingi ya dini na kusisitiza kuwa Wabahrain hawatowacha kutekeleza wajibu wao wa kimaanawi.
Ikumbukwe kuwa hivi karibuni nchi 35 wanachama wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa zililaani hatua zinazochukuliwa na serikali ya Bahrain dhidi ya wapinzani, wanaharakati na viongozi wa kidini nchini humo.
Tangu mwaka 2011 Bahrain imekuwa uwanja wa maandamano ya wananchi dhidi ya utawala wa kifalme wa kizazi cha Aal Khalifa. Wabahrain wanataka kupewa uhuru, kuondolewa dhulma na ubaguzi na kupewa haki yao ya kimsingi ya kuchagua serikali wanayoitaka wao wenyewe badala ya kutawaliwa na kizazi cha Aal Khalifa.