Mgogoro wa Syria na ukwamishaji wa viongozi wa Marekani
-
Staffan de Mistura, mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Syria.
Marekani imekuwa ikifanya njama mbalimbali za kukwamisha jitihada za kuutafutia ufumbuzi wa kisiasa mgogoro wa nchi ya Kiarabu ya Syria, suala ambalo limewafanya maafisa wa Umoja wa Mataifa washindwe kuvumilia na kuamua kuilalamikia Marekani kwa njama zake hizo.
Mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Syria, Staffan de Mistura ameilaumu Marekani kwa kuvuruga ushirikiano wake na Russia kuhusu mgogoro wa Syria na kusema kuwa, kitendo cha Marekani cha kukwamisha ushirikiano wa nchi hizo mbili ni pigo kubwa kwa jitihada za kumaliza mapigano nchini Syria. Muda wote huu viongozi wa Washington wamekuwa wakikwamisha mazungumzo yao na Russia kuhusiana na mgogoro wa Syria.
Hivi karibuni na bila ya kutarajiwa, Marekani ilitangaza kuwa imesimamisha mazungumzo yake yote na Russia kuhusiana na Syria. Kabla ya hapo Russia na Marekani zilikuwa zimefikia makubaliano ya kutekeleza usitishaji vita huko Syria. Hata hivyo makublaiano hayo hayakudumu kutokana na ukwamishaji wa kila namna wa Marekani. Miongoni mwa vipengee vilivyokuwemo kwenye makubaliano hayo ya Russia na Marekani, ni kukubali viongozi wa Washington kutoa orodha ya makundi wanayodai ni ya wapinzani wenye misimamo ya wastani huko Syria, ili kwa njia hiyo iwezekane kupambana na magenge ya kigaidi yanayofanya jinai za kila namna katika nchi hiyo ya Kiarabu. Hata hivyo Marekani kama kawaida yake, imekanyaga vipengee vya makubaliano hayo kwa kushindwa kuainisha ni makundi yapi ni ya wapiganzani wa kweli na yepi ni ya magaidi. Wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, si rahisi kwa Marekani kufanya jambo hilo, kwani dola hilo la kibeberu linayaunga mkono magenge ya kigaidi na halafu kuwadanganya walimwengu kuwa magenge hayo ni ya wapinzani wa kawaida tu wa serikali ya Syria.
Wachambuzi hao wa masuala ya kisiasa wanagusia pia misimamo ya kindumilakuwili ya Marekani kuhusiana na Syria na kubainisha kuwa, ushindi wa mfululizo wa jeshi la Syria na waitifaki wake dhidi ya magenge ya kigaidi nchini Syria umeitia kiwewe Washington na waitifaki wake na kuwafanya wasijue la kufanya. Hatua ya Marekani na kundi lake ya kuonesha chuki za wazi dhidi ya ushindi wa serikali ya Syria katika vita dhidi ya ugaidi, inazidi kuwathibitishia walimwengu kuwa Marekani haina nia kabisa ya kupambana na ugaidi. Kitendo cha hivi karibuni cha Marekani cha kutangaza kukata mazungumzo yake yote na Russia kuhusiana na Syria, ni ushahidi mwingine wa kuonesha kuwa Washington haipendi kuona mgogoro wa Syria unatatuliwa na magenge ya kigaidi yanafurushwa nchini humo.
Ikumbukwe pia kuwa, hivi karibuni Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilitangaza kuwa, Washington inachunguza njia za kuchukua hatua za upande mmoja za kuamiliana na mgogoro wa Syria. Hilo lilihesabiwa na wachambuzi wa mambo kuwa ni tishio la moja kwa moja la kufanya mashambulizi makubwa ya kijeshi nchini Syria. Inaonekana ni kwa sababu hiyo ndio maana Russia ikaionya Marekani na waitifaki wake kuwa, haziwezi kukabiliana na mfumo wa kujilinda na makombora wa Russia, na kwamba shambulio lolote lile dhidi ya maeneo ya wanajeshi wa Syria linaweza kuleta madhara kwa wanajeshi wa Russia na Syria kwa pamoja, jambo ambalo Moscow haiwezi kulinyamazia kimya hata kidogo.
Kwa kweli mgogoro wa Syria ni tata sana lakini jambo linalozidisha utata kwenye mgogoro huo, ni uingiliaji wa madola ya kigeni katika masuala ya ndani ya nchi hiyo na kuendelea kudhaminiwa kifedha na kisiasa magenge ya kigaidi; masuala ambayo Marekani inahusika moja kwa moja. Wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, mgogoro wa Syria hautoweza kumalizika kirahisi madhali madola ya kibeberu yakiongozwa na Marekani yanaendelea kuyaunga mkono magenge ya kigaidi. Kama ambavyo wanasisitiza pia kuwa, watu pekee wenye haki ya kuamua mustakbali wa Syria ni wananchi wenyewe wa nchi hiyo, hivyo madola ya kibeberu yanapaswa kutoa mkono wao haraka iwezekanavyo katika mgogoro wa Syria ili iwe rahisi kuutatua.