Saudia yasimamisha makubaliano ya kusafirisha mafuta Misri
Katika kile kinachoonekana ni kutokota mzozo kati ya Riyadh na Cairo juu ya visiwa vya kiistratajia vya Tiran na Sanafir, Misri imetangaza rasmi kuwa, Saudi Arabia imesimamisha makubaliano ya kusafirisha mafuta katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.
Tarek El Molla, Waziri wa Mafuta wa Misri amesema kuwa, licha ya kuwa, muda wa makubaliano ya dola bilioni 23 za Marekani kati ya nchi hiyo na Saudia haujakwisha, lakini utawala wa Riyadh umesimamisha kwa muda usiojulikana mpango wa kutuma mafuta yaliyosafishwa katika nchi hiyo ya Kiafrika pasina kutoa sababu zozote.
Katika makubaliano hayo yaliyofikiwa mwezi Aprili mwaka huu wakati wa safari ya Mfamle wa Saudia nchini humo, Riyadh ilikubali kusafirisha tani laki saba za mafuta yaliyosafishwa nchini Misri kila mwezi kwa muda wa miaka mitano. Imearifiwa kuwa, yumkini mzozo juu ya visiwa viwili vya Sanafir na Tiran milki ya Misri, ndio chanzo cha kuingia doa uhusiano wa nchi mbili hizi.
Hatua ya Rais Abdul Fattah al-Sisi wa Misri ya kumpatia Mfalme Salman bin Abdulaziz wa Saudia visiwa vya Sanafir na Tiran na kudai kuwa, michoro ya mipaka baharini inaonyesha kwamba, visiwa hivyo vilivyoko Bahari Nyekundu viko katika maji ya Saudia, ilipokewa kwa hasira na wananchi wa Misri walioingia barabarani na kufanya maandamano kwa siku kadhaa.
Mapema mwezi uliopita, mahakama moja nchini Misri ilianza kusikiliza rufaa ya serikali ya Cairo ya kupinga uamuzi wa mahakama ya chini ya nchi hiyo wa kutaka Saudi Arabia ipokonywe visiwa vya kistratajia vya Tifan na Sanafir, milki ya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.