Syria yajibu madai ya nchi za Magharibi kuhusu silaha za kemikali
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i20452-syria_yajibu_madai_ya_nchi_za_magharibi_kuhusu_silaha_za_kemikali
Syria imekadhibisha madai yaliyotolewa na nchi za Magharibi zinazodai kuwa, jeshi la nchi hiyo limetumia silaha za kemikali katika mapambano yake dhidi ya makundi ya kigaidi.
(last modified 2026-02-25T03:34:48+00:00 )
Nov 30, 2016 00:43 UTC
  • Syria yajibu madai ya nchi za Magharibi kuhusu silaha za kemikali

Syria imekadhibisha madai yaliyotolewa na nchi za Magharibi zinazodai kuwa, jeshi la nchi hiyo limetumia silaha za kemikali katika mapambano yake dhidi ya makundi ya kigaidi.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria, Faisal al Miqdad amesema kuwa, tuhuma mbalimbali zinazotolewa na nchi za Magharibi dhidi ya Syria kwamba imetumia silaha za kemikali dhidi ya magaidi bila ya kutoa ushahidi wa maana ni sehemu ya propaganda chafu, za kukaririwa na zinazofanyika kwa mpangilio na malengo maalumu. 

Faisal al Miqdad amepinga matokeo ya tume ya uchunguzi ya Umoja wa Mataifa iliyodai kuwa, jeshi la Syria limetumia gesi ya klorini na kusema: Ripoti hiyo imetegemea taarifa zisizo sahihi na zisizokubalika ambazo zinashusha hadhi ya Shirika la Kuzuia Silaha za Kemikali (OPCW).

Mamia wameuawa nchini Syria katika mashambulizi ya silaha za sumu ya kundi la Daesh

Tuhuma hizo za nchi za Magharibi dhidi ya Syria zimetolewa katika hali ambayo miaka kadhaa iliyopita serikali ya Damascus ilikabidhi mada zake zote za kemikali kwa Jumuiya ya Kuzuia Silaha za Kemikali (OPCW) kupitia maazimio ya Baraza la Usalama, na Umoja wa Mataifa pia umekiri kuwa Damascus imetoa ushirikiano mzuri katika uwanja huo. Migongano hiyo ya jumuiya za kimataifa kuhusu mgogoro wa Syria imesababishwa na propaganda na mashinikizo ya nchi za Magharibi kwa jumuiya hizo. Nukta ya kuzingatiwa zaidi ni kuwa, magaidi walioko Syria ambao wanaungwa mkono na kusaidiwa na nchi za Magharibi na washirika wao wa Kiarabu wanafanya jitihada za kuficha na kufunika jinai zinazofanywa na makundi hayo na kuzihusisha na serikali ya Syria. Ni kwa kutilia maanani uhakika huo ndipo Jumuiya ya Kuzuia Silaha za Kemikali (OPCW) tarehe 11 Novemba ikachukua maamuzi dhidi ya Syria kutokana na satua na ushawishi mkubwa wa baadhi ya nchi wanachama wake.

Hii ni pamoja na kuwa, ushahidi wa kutosha umethibitisha kwamba, makundi ya kigaidi kama Daesh ndiyo yanayotumia silaha za kemikali na za sumu katika nchi za Syria na Iraq, na suala hilo limekuwa likifumbiwa macho na jumuiya mbalimbali za kimataifa. Si hayo tu, bali hata nchi kama Uturuki ambayo ilikuwa miongoni mwa nchi zilizoyasaidia makundi ya kigaidi huko Syria, hivi karibuni ilikiri kuwa makundi hayo yanatumia silaha za kemikali dhidi ya raia.

Silaha za sumu zinazotumiwa na magaidi dhidi ya raia Syria na Iraq

Matukio ya sasa ya Syria ambayo yanakwenda sambamba na kubadilika kwa mlingano wa nguvu kwa maslahi ya serikali ya Damascus na wananchi na vilevile mafanikio ya jeshi la nchi hiyo katika medani za vita dhidi ya magaidi wanaosaidiwa na Wamagharibi na vibaraka wao wa Kiarabu hususan katika mji wa Aleppo, ni kielelezo cha kuanza duru mpya ya njama na propaganda mpya dhidi ya nchi hiyo. 

Madai hayo dhidi ya Syria yametolewa baada ya vyombo vya habari, kwa kutegemea ushahidi na nyaraka za kuaminika na misaada ya nchi za Magharibi kwa magaidi, vikatahadharisha juu ya uwezekano wa kufanyika mashambulizi ya kigaidi kwa kutumia silaha za kemikali. Kwa msingi huo duru za habari za Syria zinasema lengo la waungaji mkono wa makundi ya kigaidi la kutoa madai kama hayo yasiyo na msingi dhidi ya serikali ya Damascus ni kuanzisha propaganda chafu na kuyatayarishia makundi ya kigaidi mazingira mazuri ya kutumia silaha zaidi za kemikali ili kuepusha kushindwa kikamilifu katika mapambano ya Aleppo. Hapa inatupasa kusisitiza kuwa, hatua ya nchi za Magharibi na washirika wao wa Kiarabu ya kuyapa silaha za mauaji ya umati makundi ya kigaidi kwa lengo lolote lile, ni kinyume na sheria na makubaliano ya kimataifa. Makubaliano hayo yanapiga marufuku aina yoyote ya uzalishaji na usambazaji wa silaha za mauaji ya halaiki.

Faisal al Miqdad

Kwa msingi huo Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria, Faisal al Miqdad, ametahadharisha kuhusu hadaa zinazofanywa na makundi ya kigaidi na mabwana zao wa Kimagharibi na Kiarabu, na ameitaka jamii ya kimataifa kuchukua hatua kubwa na muhimu za kuzuia mashambulizi ya silaha za kemikali yanayofanywa na makundi hayo.